
Mdau maarufu wa soka kutoka mkoani Geita, Hussein Makubi Mwananyanza, ambaye pia ni mdhamini wa goli la Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan na mwanachama wa klabu ya Yanga, ametoa wito kwa wachezaji wa klabu ya Simba SC kuhakikisha wanacheza kwa juhudi na bidii kwenye mchezo wao dhidi ya RSB Berkane utakaopigwa kesho katika Uwanja wa Amani, Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Geita, Mwananyanza aliwataka wachezaji wa Simba kuacha visingizio visivyo na tija na kuelekeza nguvu zao katika mchezo, akisisitiza kuwa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hivyo hakuna sababu ya kuwa na hofu au kisingizio cha uwanja.
“Mpira hauna uchawi, bali ni suala la ufundi na maandalizi bora. Nawaomba Simba wasajili wachezaji wenye ubora na waache propaganda za ushirikina,” alisema Mwananyanza.
Aidha, aliahidi kutoa motisha ya shilingi laki tano kwa kila goli litakalofungwa na timu yoyote itakayofanya vizuri katika mchezo huo, kama njia ya kuhamasisha ushindani na mchezo wa haki.