Farida Mangube, Morogoro
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Prof. William Mwegoha, amepongeza hatua ya kuanzishwa kwa timu ya mpira wa miguu ya wanawake chuoni, akisema ni ishara ya maendeleo na usawa wa kijinsia katika sekta ya michezo ya vyuo vikuu nchini.
Prof. Mwegoha ametoa kauli hiyo wakati wa uzinduzi Mashindano ya Vitivo ya mwaka 2025 chuoni hapo, yaliyofanyika katika viwanja vya michezo vya chuo yakiwa na lengo la kukuza vipaji, mshikamano na afya miongoni mwa wanafunzi kutoka vitivo na skuli mbalimbali.
“Kuanzishwa kwa timu ya wanawake ni hatua ya kipekee katika kuleta usawa kwenye michezo. Tunataka kuona wanawake wakishiriki kikamilifu kama wenzao wa kiume. Ndoto yangu ni kuona Mzumbe ikiibuka mshindi kwenye mashindano ya kitaifa na hata kimataifa,” alisema Prof. Mwegoha kwa msisitizo.
Aidha Prof. Mwegoha aliwapongeza wanafunzi kwa mwitikio mkubwa na ari ya kushiriki mashindano, akisisitiza kuwa michezo si tu burudani bali ni nyenzo ya kujenga nidhamu, afya bora na mshikamano wa kijamii.
“Chuo kiko tayari kuwekeza zaidi kwenye miundombinu ya michezo. Naahidi msimu ujao kutakuwa na maboresho makubwa kwenye viwanja na vifaa,” aliongeza.
Kwa upande wa Serikali ya Wanafunzi kupitia Wizara ya Michezo (MUSO) iliwasilisha mapendekezo la kuanzishwa kwa kituo cha sanaa na michezo, uboreshaji wa viwanja kwa kuweka taa, na kuongeza walimu wa michezo ili kuendeleza vipaji chuoni.
Nae Kaimu Naibu Makamu Mkuu wa Chuo – Fedha, Mipango na Utawala, Dkt. Moses Ndunguru, alisisitiza kuwa michezo ni sehemu ya kujifunza maadili na ustawi wa kijamii.
“Nampongeza Prof. Mwegoha kwa kuipa michezo kipaumbele. Michezo huchangia katika ukuaji wa wanafunzi kwa njia nyingi zaidi ya darasani,” alisema Dkt. Ndunguru.
Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Wanafunzi, Bw. Alphonce Kauky, alisema mashindano hayo yanalenga kuibua vipaji, kuimarisha afya ya akili na kuunganisha wanafunzi kutoka kada mbalimbali.
“Tunawatia moyo wanafunzi – hasa wanawake – kujitokeza kwa wingi kushiriki michezo. Tupo hapa kukuza vipaji na kuimarisha umoja wetu,” alisema Bw. Kauky.
Katika siku ya uzinduzi, timu ya mpira wa miguu ya wanawake – Mzumbe Queens – iliandika historia kwa kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya timu ya Ladies. Mechi nyingine ni ya wanaume kati ya Staff na Kitivo cha Sheria (Law) iliyomalizika kwa sare ya bila kufungana, na mpira wa kikapu kati ya Staff na Skuli ya Biashara (SoB) ambapo SoB waliibuka washindi.
Mashindano haya, yaliyoanza Mei 17 na kutarajiwa kufikia tamati Juni 1, 2025, yanajumuisha michezo mbalimbali kama mpira wa miguu, pete, kikapu, wavu, riadha na mingineyo. Ushiriki mkubwa wa wanafunzi unadhihirisha dhamira ya kweli ya Chuo Kikuu Mzumbe kukuza vipaji na kuendeleza michezo kama sehemu ya maendeleo ya kitaaluma na kijamii.