NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
CHUO Kikuu cha Dar es salaam (UDSM) kwa kushirikiana na Watumishi Housing Investment (WHI),wamesaini mkataba wa makubaliano wa ujenzi na uendeshaji wa jengo la kisasa la Biashara chuoni hapo ili kuongeza ufanisi wa huduma kwa jamii.
Akizungumza na habari leo Mei 26, 2025 Jijini Dar es Salaam, Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Prof. William Anangisye amesema ujenzi wa jengo hilo litakuwa kitega uchumi kutokana na kuwa na ofisi, maduka na maeneo ya michezo ya watoto.
Amesema ujenzi huo utagharimu kiasi cha shilingi bilioni 8.3 na natarajiwa kukamilika kwa kipindi cha miezi 18
Prof. Anangisye amesema pindi ujenzi utakapokamilika, jengo litakuwa na maeneo ya kutolea huduma mbalimbali kwa ajili ya wanafunzi, wafanyakazi na wananchi kwa ujumla.
“Huduma hizo zitajumuisha kumbi za mikutano, Executive lounge, Supermarket, Executive Car Wash, Migahawa, Kumbi za mazoezi ya viungo (Gym), Huduma za udobi, Vyumba vya ofisi na michezo ya watoto”. Amesema Prof. Anangisye.
Kwa upande wake Kaimu Afisa mtendaji mkuu wa Taasisi ya watumishi Housing Sephania Solomon amesema matarajio katika kipindi cha miaka kumi na tano jengo hilo litaingia zaidi ya shilingi bilioni15 ambapo Chuo Kikuu itapata asilimia 40 na Taasisi ya Watumishi House itapata asilimia 60.