Rais wa Jumuiya ya Kimataifa Wahandisi wa Petroli Society of Petroleum Engineers International (SPEI)), Olivier Houze akitoa histori ya petroli duniani katika mkutano wa Africa Techinology unaoendelea kufanyika jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, akizungumza leo Mei 27, 2025 jijini Dar es Salaam na waandishi wa habari mara baada ya kufungua mkutano wa Africa Teknology.
Mhandisi Mwandamizi wa Petroli – TPDC, Modestus Lumato akizungumza kuhusiana na fursa zilizopo hapa nchini akizungumza katika mkutano wa Africa Technoloji unaoendelea kufanyika jijini Dar es Salaam.
NI muhimu kuwaandaa vijana na wataalamu wa sekta ya Petroli ili kuendana na kasi ya mabadiliko ya teknolojia katika sekta ya petoli yanayoendelea duniani.
Kauli hiyo imetolewa leo Mei 27, 2025 jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA), Mhandisi Charles Sangweni, katika mkutano wa Africa Technology, unaokutanisha Wakurugenzi wa Petroli kutoka nchi mbalimbali za Afrika pamoja na wanafunzi wa vyuo wanaosoma masuala ya petroli. Mkutano huu unalenga kutoa fursa ya kubadilishana uzoefu na kuelekezana kuhusu mustakabali wa sekta ya mafuta na nishati duniani.
Mhandisi Sangweni amesema kuwa mkutano huo wa siku mbili unahusisha wataalam na wadau wa sekta ya mafuta na nishati kutoka kote duniani, na unatoa fursa ya kipekee kwa Afrika, hususan Tanzania kuelezea dira yake katika safari ya kuelekea matumizi ya nishati safi na endelevu.
Akizungumzia jitihada za kitaifa, Mhandisi Sangweni amepongeza uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan na Naibu Waziri Mkuu ambaye pia ni Waziri wa Nishati, Dkt. Mashaka Biteko, kwa kuongoza juhudi za utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia, upatikanaji wa umeme vijijini, na uboreshaji wa elimu kupitia nishati.
Ameeleza kuwa miradi hiyo haishughulikii tu changamoto za usalama wa nishati, bali pia inavutia wawekezaji wapya na kuchochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi nchini.
Aidha, Mhandisi Sangweni ametoa wito kwa wawekezaji wa kimataifa kuja kuangalia fursa zilizopo nchini Tanzania, hasa katika sekta ya mafuta na gesi, pamoja na miradi ya nishati mbadala. Amebainisha kuwa, zaidi ya mitaji, Tanzania inahitaji ushirikiano wa kimkakati na uhamishaji wa maarifa ili kufikia teknolojia ya kisasa inayohitajika kuendeleza sekta hiyo.
Katika hotuba yake, pia amesisitiza mchango mkubwa wa Jumuiya ya Wahandisi wa Petroli (SPE) Afrika na Tanzania katika kufanikisha mkutano huo na kuunda jukwaa la kujadili changamoto na suluhisho katika sekta ya petroli. Akiwa na matumaini makubwa kwa siku zijazo, Mhandisi Sangweni al inukuliwa akisema:
“Afrika ni kanda inayochangamka na kujaa fursa – tunapaswa kuchukua hatua sasa kwa maendeleo ya baadaye.”
Kwa upande wa Mkurugenzi wa Kanda ya Afrika Dkt. Riverson Oppong amesema kuwa wapo tayati kuungana nchi zote za Afrika kuangalia fursa zilizopo nchini ili kuja kuwekeza katika sekta ya Petroli.
Mwenyekiti wa jumuiya ya wafanyakazi wa Petroli (SPEI) Tanzania, Alex Buko amesema kuwa amesema mkutano huo unaotazamia masuala ya teknolojia katika sekta ya petroli Afrika umefanikiwa pia amewashukuru wadhamini na serikali ya Tanzania pamoja na Wizara ya nishati kwa kupitia taasisi zake ambazo ni PURA, TPDC Ewura na wadau mbalimbali wanaofanya shughuli za mafuta hapa nchini ambao wameshirikiana nao kwa kiasi kikubwa kufanikisha mkutano huo.
Amesema mkutano huo utakuwa na manufaa mengi ikiwa ni pamoja na kutoa fursa za utalii na baada ya mkutano huo baadhi ya wageni watatembelea Zanzibar kwaajili ya kuona vivutio vilivyopo hapa nchini.
Kongamano hili limefungua ukurasa mpya wa ushirikiano, uboreshaji wa maarifa, na uwekezaji kwa mustakabali wa nishati endelevu barani Afrika. PURA, kama taasisi ya udhibiti wa rasilimali za mafuta nchini Tanzania, iko tayari kuendelea kuongoza kwa maono, mshikamano, na ushirikiano wa kimataifa.
