Mtwara
Serikali kupitia Wizara ya Maji imetoa kiasi cha Shilingi 815,453,185 kwa ajili ya ukarabati wa Mradi wa Maji Dihimba, unaolenga kuwahudumia wakazi zaidi ya 7,489 wa vijiji vya Dihimba, Mpondomo, Kinyamu na Ndumbwe vilivyopo Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara, Mkoani Mtwara.
Kwa mujibu wa Meneja wa Wakala wa Usambazaji Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA) Wilaya ya Mtwara, Hamis Mashindike, kati ya fedha hizo Shilingi 694,271,895 zimetumika kumlipa mkandarasi, huku Shilingi 121,181,200 zikitumika kwa ununuzi wa mabomba kutoka RUWASA Makao Makuu kupitia kampuni ya M/S Zonghi Plumbing & General Supplies Company Ltd.
Mashindike amesema ukarabati wa mradi huo ulianza Januari 2024 na ulitarajiwa kukamilika Septemba mwaka huo, lakini kucheleweshwa kwa malipo ya hati ya madai pamoja na mvua nyingi kumesababisha ucheleweshaji wa kazi, hivyo muda umeongezwa na mradi unatarajiwa kukamilika Juni 2025.
Mradi huo, unaotekelezwa na mkandarasi M/S Seba Construction, tayari umefikia asilimia 75 ya utekelezaji na mkandarasi amelipwa Shilingi 100,766,635.90 kama malipo ya awali.
=Ukarabati huo umehusisha ujenzi wa tanki moja la kuhifadhi maji lenye ujazo wa lita 100,000 katika kijiji cha Mpondomo na ukarabati wa matenki mawili ya lita 200,000 katika kijiji cha Ndumbwe. Vilevile, vituo 17 vya kuchotea maji vimejengwa, pamoja na nyumba ya mhudumu na ofisi ya Jumuiya ya Watumia Maji ngazi ya jamii (CBWSO).
Aidha, mabomba yenye urefu wa kilomita 9.74 yamenunuliwa na mkandarasi, na RUWASA Makao Makuu imepeleka mabomba yenye urefu wa kilomita 14.781 kwa ajili ya ulazaji.
Mashindike amesema faida za mradi huu ni pamoja na kuongezeka kwa upatikanaji wa maji safi na salama kutoka asilimia 37.04 hadi asilimia 93.47 ifikapo mwaka 2025, sawa na ongezeko la asilimia 56.43. Mradi pia umetatua changamoto ya upatikanaji wa maji katika vijiji husika, kupunguza magonjwa ya mlipuko, na kuchangia ajira za muda mfupi na mrefu kwa wananchi.
Vituo vya kuchotea maji vimezingatia sera ya “Kumtua mama ndoo kichwani” kwa kuweka umbali usiozidi mita 400 kutoka kituo kimoja hadi kingine. Hadi sasa, kaya 48 na taasisi mbili za umma zimeunganishwa na huduma ya maji.
Mkuu wa Mkoa wa Mtwara, Patrick Sawala, amesema mradi huo ulizinduliwa mwaka 1989 lakini haujawahi kufanyiwa ukarabati hadi sasa. Kwa sasa mradi huo umewezesha wananchi kupata maji ya uhakika na kupunguza adha ya kutembea umbali mrefu.
Ameongeza kuwa mkoa wa Mtwara unaendelea kutekeleza miradi mingine mikubwa na midogo ya maji, ikiwemo Mradi wa Maji wa Miji 28 wa Mto Ruvuma, ambao unatarajiwa kuhudumia miji ya Mangaka, Masasi na Nachingwea mkoani Lindi.
Mkazi wa kijiji cha Dihimba, Mwanahawa Rashid, ameishukuru Serikali kwa ukarabati huo na kusema awali walilazimika kutembea hadi kilomita tatu kutafuta maji, lakini sasa huduma hiyo inapatikana kwa urahisi kijijini