NA MWANDISHI WETU
MTENDAJI Mkuu wa Vertex International Securities limited Mateja Mgeta amewataka watu kuwekeza kupitia huduma ya Vertex Mobile Trading App ambayo itawasaidia wananchi kufanya uwekezaji kwa wepesi kwa kuwa ni moja ya njia nyepesi kwa watumiaji.
Mateja amebainisha hayo leo Jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa Vertex Mobile Trading App yenye lengo la kuwapa wepesi wawekezaji kupitia simu janja zao.
Amesema lengo la ujio wa app hiyo una sura mbili ambazo ni kuwapa watu maarifa ya uwekezaji kwa urahisi iwe mtu anahitaji kuwekeza hisa katika makampuni yaliyoorodheshwa na soko la hisa la Dar es Salaam (DSE) hivyo imani ni kubwa kuwa elimu ndio funguo ya ushiriki wa uwajibikaji.
Sababu ya pili iliyowasukuma kuanzisha Vertex Mobile Trading App kulenga kurahisisha mfumo wa uwekezaji kuufanya uwe wazi, rahisi na salama kwa watumiaji ambao mwekezaji au mwekezaji mtarajiwa anayetumia simu janja (smart phone) anaweza kufungua akaunti ya hisa, kununua au kuuza hisa kupitia kiganjani pasipokuwa na ulazima wa kufika ofisni kwao.
“Masoko ya mitaji yana jukumu muhimu sana katika kukusanya fedha kwa ajili ya matumizi yenye tija yanayotumika kama njia ambazo akiba inaweza kuelekezwa kwenywe miradi inayochochea ukuaji wa uchumi, ubunifu na kutengeneza ajira,”amesema Mateja.
Aidha Mateja amesema uwekezaji uchangia kikamilifu katika ajenda ya uchumi wa Taifa, hivyo kutokana na uwekezaji unaweza kuimalisha masoko ya mitaji ya ndani, kupunguza utegemezi wa ufadhili kutoka nje na kukuza uwekezaji utakaochochea ustawi wa pamoja.
Mateja ametoa pongezi kwa mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana Tanzania (CMSA) chini ya Mtendaji wake Mkuu CPA Nicodemus Mkama kwa kuweka mazingira wezeshi katika soko kwani bila miongozo yao wasingeweza kufika walipo sasa.
Pia alitoa pongezi kwa Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) chini ya Afisa Mtendaji Mkuu Peter Nalitolela kwa mchango wao mkubwa kuhakikisha Vertex Mobile Trading App mafanikio ya hisa kiganjani ambayo yamefanywa na wao Vertex International Securities limited.
Kwa upande wa mwakilishi kutoka CMSA Alfred Mkombo amesema wao mamlaka ya msoko ya mitaji wanafurahi kuona maendeleo kama haya ambayo yanawapa watu urahisi wa kuwekeza kupitia simu zao viganjani.
“Simu imekuwa kitu kikubwa zipo hadi vijijini mtu anaweza kushiriki minada inayotokea Dar es Salaam bila kusafiri na kutumia gharama kubwa, Vertex Mobile App imetengenezwa ili kuleta mageuzi na ni tekinolojia ambayo inatumika kwa wepesi bila hata kutumia nguvu,”
“Tunapenda kuona teknolojia hizi zinaleta tija zaidi tunawapongeza sana Vertex kwa namna ya kipekee kufikia hatua hii kubwa sana ya mafanikio ambayo inaakisi sera na sheria usimamizi unaoleta mazingira bora,”amesema Mkombo.
Huku Ali Othman kutoka DSE amesema jambo lililofanywa na Vertex ni kubwa na litaleta mafanikio makubwa kwa kuwa ni njia nzuri na rahisi kwa watu kutumia.
“App ina kila kitu kwa mtumiaji wa mtandao wowote Vertex Mobile Trading App imewarahisishia hii ni hatua nzuri inaongeza ushindani na ubunifu mpya kwa watu wote kuwekeza iwe mjini na hata vijini,”amesema Othman.