Na Mwandishi Wetu, Manyara
MAADHIMISHO ya wakulima wa NOURISH yaliochukua wiki nne kwa nyakati tofauti katika halmashauri za wilaya 10 Tanzania, yamefikia tamati katika Wilaya Babati na kufikia wakulima maelfu kupitia elimu ya kilimo chenye tija na lishe bora.
Wilaya ya Babati imehitimisha kilele cha maadhimisho hayo ambayo yalianza mnamo mwishoni mwa mwezi wa nne kwa kuleta pamoja wakulima na wadau mbalimbali wa kilimo kujifunza na kusherehekea mafanikio ya mradi wa NOURISH wilayani humo.
Akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Endanoga Wilaya ya Babati ambapo maadhimisho hayo yalifanyika, Ofisa Mradi wa NOURISH, Salome James, kutoka katika Shirika la RECODA aliweka bayana kuwa mradi ulianza utekelezaji wake wilayani humo mwishoni
mwa mwaka 2024 na hadi sasa umefanikiwa kwa sehemu kubwa, kuwawezesha wakulima kujifunza kwa vitendo kanuni bora za kilimo chenye tija kinachostahimili mabadiliko ya tabia nchi kupitia mashamba darasa, pamoja na kuwaunganisha wakulima wadogo na kampuni zinazozalisha na kusambaza pembejeo bora za kilimo.
“Mpaka sasa tumefanikiwa kuanzisha vikundi vya kilimo 75 vikiwa na jumla ya wanachama 2,346, mashamba darasa 57, kusambaza Mbegu za viazi lishe kwa lengo la kuzalisha mbegu kwenye ngazi ya kata ambapo jumla ya pingili 40,000 zimekwishatolewa,“ amesema Salome.
Naye Katibu Tawala wa Wilaya ya Babati, Khalfan Matipula, alipongeza mradi wa NOURISH kwa mradi kuwaongezea ujuzi wahudumu wa afya ngazi ya jamii ambao wamekua chachu katika kutoa elimu ya afya na lishe katika jamii zetu ili kupunguza tatizo la utapiamlo haswa udumavu kwa Watoto na kusisitiza wakulima washiriki wa mradi kuwa chachu ya maendeleo kwa kutekeleza kwenye kaya zao yale waliyojifunza na kushiriki katika vikundi na wataalamu wa kilimo na wakulima viongozi (lead farmers) pamoja na wahudumu wa afya ngazi ya jamii.
“Maisha bora yanapatikana kwa kila mmoja kufanya kazi kwa bidii na kwa kutumia utaalamu. Nishauri tena wataalamu wa ugani hakikisheni mnawajibika kuleta maendeleo hasa kwa kwenda na hili wimbi la mradi huu ambao umeonyesha njia ya kweli ya maendeleo vijijini.” Khalfan Matipula.
Mradi wa NOURISH wilayani Babati unatekelezwa katika vijiji 42 vilivyoko katika kata 10 ambapo utekelezaji wa mradi huu, mashirika wabia wamekuwa wakitumia maafisa ugani, wahudumu wa afya ngazi ya jamii na wakulima viongozi wa ngazi ya kijiji ambao walichaguliwa na serikali za vijiji na kupewa mafunzo juu ya utekelezaji wa kazi zao kabla ya kuanza kufanya kazi za mradi.