Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA), kwa kushirikiana na Benki Kuu ya Tanzania (BOT), imeandaa semina ya pamoja uliyowakutanisha wataalamu wa uhasibu, wakaguzi wa hesabu na wadau wa sekta ya fedha kutoka ndani na nje ya nchi.
Akifungua rasmi semina hiyo iliofanyika jijini Arusha, Gavana wa BOT, Emmanuel Tutuba, alisisitiza umuhimu wa taaluma ya uhasibu katika kuchochea maendeleo ya uchumi wa taifa. Alitoa wito kwa wahasibu na wakaguzi kutumia maarifa yao kuboresha uwajibikaji wa kifedha katika taasisi zote za umma na binafsi.
“Tunahitaji uadilifu, uwazi, na matumizi ya teknolojia katika usimamizi wa fedha. Hili linaanza na taaluma ya uhasibu,” alisema Tutuba.
Semina hiyo yenye kaulimbiu: “Utawala Bora na Uwajibikaji Katika Mazingira ya Kidigitali”, unalenga kuangazia nafasi ya taaluma ya uhasibu katika ulimwengu unaoongozwa na TEHAMA na akili bandia (AI).
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno, alisema taasisi hiyo inaendelea kusimamia ubora wa huduma za uhasibu nchini kwa kuweka mifumo ya kisasa ya udhibiti na usimamizi wa taarifa za kifedha.
Alibainisha kuwa NBAA imeanzisha mfumo mpya wa kudhibiti uwasilishaji wa hesabu, ambapo wakaguzi wote watatakiwa kuwasilisha taarifa NBAA kwa ajili ya kupata namba ya uthibitisho kabla ya kutumika rasmi na taasisi husika.
Semina hiyo ya siku tatu imehudhuriwa na washiriki takribani 800 wakiwemo wahasibu wakuu, wakaguzi wa ndani na nje, wakufunzi wa vyuo, pamoja na wadau wa sekta ya fedha na biashara.
Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BOT), Emmanuel Tutuba akizungumza wakati wa kufungua semina kati ya Bodi ya Taifa ya Wahasibu na Wakaguzi wa Hesabu Tanzania (NBAA) na BOT iliyofanyika jijini Arusha
Mkurugenzi Mtendaji wa NBAA, CPA Pius Maneno akizungumza wakati wa ufunguzi wa semina kati ya NBAA na BOT iliyowakutanisha wataalamu wa uhasibu, wakaguzi wa hesabu na wadau wa sekta ya fedha kutoka ndani na nje ya nchi.
Baadhi ya wataalamu wa uhasibu, wakaguzi wa hesabu na wadau wa sekta ya fedha kutoka ndani na nje ya nchi wakifuatilia ufunguzi wa semina iliyoandaliwa na na NBAA na BOT
Picha ya pamoja