Ameyasema hayo wakati wa hafla fupi ya uzinduzi wa mradi wa nishati hiyo wenye thamani shilingi bilioni 1.18, uliofanyika kiwandani hapo jana, ambapo yeye alikuwa ni mgeni rasmi.
“Mradi huu ambao ni wa kwanza na wa kipekee hapa nchini, kwakweli utakuwa suluhisho siyo tu kupunguza gharama za uendeshaji kwa wawekezaji hawa, lakini pia utasaidia kupunguza matumizi ya nishati chafu inayotokana na utumiaji majenereta hasa kunapokuwa na mgao wa umeme,” amesema.
Malima ambaye amewahi kuwa Naibu Waziri wa Nishati katika awamu zilizopita, amesema hapo awali ilikuwa ni vigumu kutumia nishati jua kwa ajili ya matumizi tu ya nyumbani, kwani iliaminika kwamba hauna nguvu za kuwasha hata friji.
“Wakati huo mimi nikiwa kule Bungeni nikiulizwa maswali kuhusu nishati hii, wataalamu wetu walikuwa wananiletea majibu kuwa umeme huo hauna nguvu,” alisema.
Amesema ameshangazwa na alichokiita ni maajabu kiwandani hapo ambapo wanazalisha nusu megawati ya nishati hiyo, ambayo inatumika kwa shuhuli zote za kiofisi na kiwandani wakati wa mchana, huku umeme wa Tanesco ukiendelea kutumika nyakati za usiku,” amesema.
Ameahidi kwamba atakuwa ni Balozi mzuri wa matumizi ya nishati hiyo, ambayo Alliance One wameanza kuitumia, ambapo amesema ataanza mara moja kuwaalika watumiaji wakubwa wa umeme mkoano Morogoro waende kiwandani hapo wakajionee mapinduzi hayo.
“Watumiaji wakubwa wa umeme mkoani kwetu wengine hutumia majenereta,ambayo huzalisha kiasi kikubwa hewa ya ukaa.Nimeambiwa kuwa ninyi pia mlikuwa mnatumia lita 7500 za dizeli kwa saa moja,lakini sasa mmeachana na hali hiyo baada kuanza matumizi ya nishati safi,sasa kwanini jambo zuri kama hili wengine wasiige ?,” amesema.
Kwa upande wake Msemaji wa Alliance One Wakili John Magoti, amesema mkakati wa kubadilisha matumizi ya nishati chafu, kwenda kwenye nishati safi, ulikuja sambamba na wito wa Rais Samia Suluhu Hasan ambaye ameweka kipaumbele matumizi ya nishati hiyo.
Amesema kinachoufanya mradi huo kuwa ni wa kipekee ni mfumo bunifu kifedha, ambapo kampuni haikulazimika kuwekeza mtaji,bali uwekezaji huo umefanywa na mbia wao ambayo ni kampuni ya Puma Energy, kwa makubaliano kwamba Alliance One watakuwa wakilipia gharama za nishati hiyo kwa kadri wanapoutumia.
“Mpango huu umetuwezesha kunufaidika na nishati safi pasipo kuwa mzigo wa fedha za mtaji na makubaliano yetu haya ni ya miaka 10;kisha baada ya hapo mradi huu tutaumiliki sisi wenyewe kwa asilimia 100,” amesema na kuongeza kuwa umri wa mradi huo ni miaka 25.
Amesema utekelezaji wa mradi huo ni matokeo ya nia thabiti ya kampuni hiyo ya kuendeleza safari ya biashara endelevu inayojali mambo matatu; yaani watu, sayari pamoja na faida.
Mradi huu kimsingi hauna lengo la kupunguza gharama za nishati pekee, bali ni mkakati wa kujikita kwetu kwenye ubunifu endelevu,huku tukifanya bisahara yenye uwajibikaji na ndiyo maana tumekuwa wa kwanza hapa nchini kutekeleza jambo hili,” amesema.
Mkuu wa Uhandisi wa Kampuni hiyo, Mhandisi Shepherd Karuwa, ambaye pia ndiye mbeba maono wa mradi huo ameeleza kuwa awali walikuwa na changamoto ya kukatika umeme mara kwa mara, hali ambayo iliwalazimu wakati mwingine kusimamisha kwa shughuli za uzalishaji kiwandani hapo.
Alisema ili kukabiliana na changamoto hiyo kampuni ikaamua kutumia jenerata la mafuta ya dizeli, ambalo nalo liliambatana gharama za uendeshaji sambamba uzalishaji wa hewa ya ukaa, hali iliyowafanya kuamua kubuni mradi huo wa nishati safi.
“Nishati hii kwanza haichafui mazingira,lakini pia gharama yake ni nafuu kuliko vyanzo vingine vya nishati, kwani hapo awali kwenye matumizi ya jenereta tulikuwa tukitumia shilingi milioni 55 kwa siku, lakini sasa matumizi ya nishati ni shilingi milioni 25 kwa siku,” amesema.