-Yasisitiza ni salama, gharama nafuu na ni rafiki wa mazingira
-Yathibitisha kuendelea kuwawezesha wazalishaji wake
Wakala wa Nishati Vijijini unahamasisha wananchi kote nchini kutumia nishati safi ya kupikia ikiwemo Mkaa mbadala ambao umeelezwa kuwa na gharama nafuu na ni salama kwa afya ya mtumiaji na mazingira.
Mkurugenzi wa Teknolojia za Nishati Jadidifu na Mbadala, Mhandisi Advera Mwijage kutoka REA ametoa wito huo Mei 31, 2025 alipotembelea na kukagua uzalishaji wa mkaa mbadala unaotokana na mabaki ya makaa ya mawe katika kiwanda cha Rafiki Briquettes kinachomilikiwa na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) kilichopo Wilaya ya Kisarawe Mkoani Pwani.
“Watanzania tusiogope mabadiliko katika matumizi ya nishati safi mbalimbali za kupikia. Mkaa unaozalishwa kutokana na mabaki ya makaa ya mawe ni salama kiafya,safi na nafuu sana katika matumizi. Leo katika Ziara hii nimetembelea hapa nimejiridhisha pasi na shaka mkaa huu ni salama kutokana na technolojia inayotumikabkatika utengenezaji ,” alisisitiza Mhandisi Advera.
Alisema REA inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati Safi ya Kupikia na miongoni mwa majukumu iliyopewa ni kuhamasisha na kuwezesha uzalishaji, usambazaji wa bidhaa za nishati safi ya kupikia ili kila mwananchi afikiwe na amudu gharama zake.
Alisema ametembelea kiwanda hicho ili kushuhudia hali ya uendeshaji wake, kujionea uzalishaji wa mkaa mbadala ili kuwaondolea baadhi ya wananchi dhana iliyojengeka miongoni mwao ya kwamba mkaa huo si salama na pia kuona namna ambavyo serikali kupitia REA itaendelea kuwezesha uzalishaji wa mkaa huo.
“Hapa ninavyozungumza tayari tumepokea maombi kutoka STAMICO ya kuwawezesha kununua mitambo mingine ili waweze kutanua wigo wa uzalishaji, nimeridhishwa na kazi inayofanyika na sisi REA tunaahidi kuendeleza ushirikiano ili kufikia lengo na dhamira ya Serikali inayoongozwa na Rais, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan,” alifafanua Mha. Advera.
Alishauri STAMICO kushirikiana na vyombo vya habari na makundi mbalimbali katika jamii katika kutoa elimu ya matumizi sahihi ya mkaa huo ili kuondoa dhana hiyo mbaya miongoni mwa jamii.
Akizungumzia malengo na hali ya uzalishaji, Kaimu Mkurugenzi wa STAMICO, Deusdedith Magala alisema kiwanda hicho kinao uwezo wa kuzalisha kiasi cha tani 20 kwa saa na kwamba mbali na kiwanda hicho cha Kisarawe, STAMICO inamiliki viwanda vingine viwili kimojawapo kikiwa Dar es Salaam eneo la Tirdo na kingine Kiwira kulipo na malighafi hiyo ya makaa ya mawe.
“Lengo letu ni kuwa na viwanda 21 Tanzania Bara ili kurahisisha ufikishaji wa bidhaa kwa wananchi kwa gharama ambayo kila mwananchi anamudu, kwa sasa kilo moja ya mkaa kwa bei ya rejareja tunauza kwa shilingi 1,000 na kwa bei ya jumla ni shilingi 800,” alisema Magala.
Alisema viwanda viwili viko mbioni kukamilika kimoja kinajengwa Mkoani Dodoma na kingine kinajengwa Mkoani Tabora kwa lengo la kupunguza ukataji ovyo wa miti unaofanywa na wakulima wa tumbaku mkoni humo wakati wa kukausha zao hilo,” alisema Magala.
Naye Mhandisi Muendeshaji wa kiwanda hicho, Goodluck Mhagama alisema mkaa huo ni rahisi ikilinganishwa na mkaa wa miti kwani kilo moja inaweza kutumika kupikia kwa zaidi ya Saa 4 bila kupunguza ukali wake.
“Kilo moja ya mkaa huu unaweza kupikia maharagwe, nyama, wali ama kusonga ugali na hata kuchemsha maji bila kuongeza mkaa mwingine, wewe kazi yako ni kubadilisha tu sufuria,” alsema Mhandisi Mhagama.
Alisema uandaaji wa mkaa huo umezingatia vigezo vyote muhimu na kwamba mkaa huo ni salama na hauna madhara yoyote kwa mtumiaji ama kwa mazingira na kwamba umethibitishwa na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).