Benki ya Taifa ya Biashara (NBC) imempogeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kufutia tuzo maalum ya heshima aliyotunukiwa na Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kuthamini kazi kubwa na nzuri aliyofanya katika kuleta maendeleo nchini.
Aidha, benki hiyo imeahidi kuendelea kuunga mkono jitihada za Rais Samia kwa kuendeleza ushirikiano wake na serikali pamoja sekta binafsi katika kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati inayotekelezwa kwa manufaa ya Watanzania kupitia huduma bora za kifedha.
Akizungumzia tuzo hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi aliyekuwa miongoni mwa wageni waalikwa katika hafla hiyo iliyofanyika leo kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma, pamoja na kumpongeza Rais Samia kwa tuzo hiyo alisema benki ya NBC inaunga mkono mafanikio hayo kwa kuendelea kubuni na kutoa huduma mbalimbali za kifedha ikiwemo mikopo na ufadhili wa miradi mbalimbali ya kimkakati.
“Tunampongeza sana Mheshimiwa Rais Samia kwa tuzo hii ya heshima inayoashiria kwamba jitihada zake katika kuchochea kasi ya maendeleo hapa nchini inaonekana na inathaminiwa pia na miimili mingine ya kitaifa. Katika kuunga mkono mafanikio haya NBC tunaahidi jitihada zaidi kwa kutoa kipaumbele kwenye kufanikisha miradi mbalimbali ya kimkakati ikiwemo ujenzi na uboreshaji wa miundombinu, sekta ya kilimo, afya, elimu, utalii, michezo na sekta nyingine muhimu,’’ alitaja.
Sabi alitolea mfano jitihada za benki hiyo ikiwa kama mtaalam mshauri katika kufanikisha uuzwaji wa hati fungani ya Mamlaka ya Maji Tanga (Tanga-UWASA) kwa ajili ya ujenzi wa miundombinu ya maji mkoani Tanga mwaka jana.
“Huo ni mfano mmoja tu kati ya mifano mingi ya miradi tunayoshiriki kuifanikisha kupitia mikopo mbalimbali kwa serikali na wazabuni, ufanikishaji wa miamala ya kifedha ikiwemo ya kimataifa, kubadili fedha za kigeni pamoja na ufadhili wetu kwenye jitihada za kijamii hususani kwenye sekta ya afya.’’ Alisema Sabi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan (kulia) akionyesha Tuzo Maalumu ya Heshima kutoka kwa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania baada ya kukabidhiwa na Spika wa Bunge hilo, Dkt. Tulia Ackson ikiwa ni ishara ya kuthamini kazi kubwa na nzuri aliyofanya katika kuleta maendeleo nchini.
Baadhi ya viongozi wa taasisi na mashirika mbalimbali hapa nchini akiwemo Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya NBC, Theobald Sabi (katikati- mstari wa mbele) wakifuatilia hafla ya utoaji tuzo ya maalum ya heshima kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt Samia Suluhu Hassan kutoka Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania iliyofanyika leo kwenye viwanja vya Bunge jijini Dodoma.