Na Mwandishi Wetu
ZAIDI ya wanariadha 6,000, wameshiriki Mbio za Hisani za Pugu Marathon 2025 zilizodhaminiwa na Benki ya NMB zenye lengo la kuchangisha fedha kusaidia maeneo yenye uhitaji mkubwa katika jamii lakini pia kuendeleza Kituo cha Hija kilichopo Pugu jijini Dar es Salaam.
Mbio hizo za Pugu Marathon ambazo huandaliwa na Kanisa Katoriki Jimbo Kuu la Dar es Salaam, zimefanyika kwa mwaka wa tatu mfululizo ambapo washiriki wamekimbia umbali tofauti tofauti wa kilometa 2.5, 5, 10 na 21 (Half Marathon) ili kujenga afya zao.
Akizungumza wakati wa mbio hizo, Askofu wa Msaidizi wa Jimbo Kuu Katoriki Dar es Salaam, Henry Mchamungu, amesema mbio hizo lengo lake ni kupata fedha za kuendeleza Kituo cha Hija cha Pugu ili kiweze kuwa na hadhi ya kimataifa pamoja na kukamilisha Jengo la Utawala la kituo hicho cha Hija.
“Mbali na hilo fedha nyingine zitakazopatikana zitasaidia kuimarisha maktaba ya Shule ya Sekondari ya Pugu alipofundisha Mwalimu Julius Nyerere,” alisema Askofu Mchamungu na kuongeza;
“Kwa hiyo niwaombe tu wadau mbalimbali kuendelea kutuunga mkono kila tutakapokuwa tunaandaa mbio hizi ambazo zitakuwa zikifanyika kila mwaka.”
Pia Ofisa Mkuu Wateja Wakubwa na Biashara za Serikali wa Benki ya NMB ambayo ndiyo wadhamini wakuu wa mbio hizo, Alfred Shao, aliupongeza uongozi mzima wa Jimbo Kuu Katoriki-Dar es Salaam kwa kuandaa mbio hizo.
Alisema waandaaji wamefanya ubunifu mkubwa wa kuandaa mbio hizo za hisani za Pugu Marathon ambazo zimefanyika kwa mafanikio, huku zikizidi kushirikisha wadau mbalimbali kuchangia fedha za kusaidia maeneo yenye uhitaji mkubwa katika jamii yetu.
“Nimefurahi kuona Watanzania wengi pamoja na wageni mmejitokeza na kushiriki Pugu Marathon ili kuchangia kuendeleza Kituo cha Hija Pugu kama mojawapo ya vivutio vya utalii ndani ya nchi, pamoja na kufanya matendo ya huruma katika hospitali, kusaidia wahitaji mbalimbali lakini pia kusaidia maktaba katika shule ya Pugu Sekondari ambayo Baba wa Taifa Mwalimu Julius Kambarage Nyerere alifundisha,” alisema Shao.
Akikumbushia aliyoyasema Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye alikuwa Mgeni Rasmi katika mbio za msimu wa pili wakati wa risala yake, alitoa maelekezo ya kuingiza kituo hicho katika orodha ya vivutio vya kitalii Tanzania.
“Nimefarijika kusikia Pugu Marathon itaendelea kuwepo na awamu ya nne hapo mwakani. Benki ya NMB kama wadau wa maendeleo na michezo tutaendelea kuwa nanyi bega kwa bega kwa kushiriki kikamilifu kwenye mbio hizi.
“Tunatambua kupitia mbio hizi kuna shule na hospitali zilizoandaliwa kupokea msaada kwa matendo ya huruma hivyo Benki ya NMB tumeguswa kuchangia vitanda na mashuka kwa ajili ya Kituo cha Afya Majohe na baskeli 6 kwa ajili ya wanafunzi wenye ulemavu wanaosoma Shule ya Sekondari Pugu vyote vikiwa na thamani ya shilingi milioni 10”.
Katika mbio hizo kwa upande wa wanaume kilometa 21, kinara alikuwa ni Edson Mwakalukwa kutoka Ukonga aliyetumia saa 1:26:19, akifuatiwa na Joseph Mlewa wa Msimbazi aliyetumia saa 1:34:58 na Francis Ngao wa Rinzudi-Goba aliyetumia saa 1:36:42.
Kwa wanawake mshindi ni Alafa Msalo kutoka Zimamoto aliyetumia saa 1:49:47, akifuatiwa na Happynes Temu aliyetumia saa 2:10: 12 na wa tatu ni Heether Steele wa Dar es Salaam aliyetumia saa 2:18:33.
Kwa upande wa kilometa 10 wanaume, mshindi ni Paschal Baloho wa Mbezi Mwisho aliyetumia dakika 36:25:37, akifuatiwa na Imlan Dadi wa Mbezi aliyetumia dakika 42:04: 27 na Dickson Mikirandi wa Kibangu aliyetumia dakika 42:29:26.
Wakati kwa wanawake washindi ni Christina George wa Dar es Salaam aliyetumia dakika 50:15:06, akifuatiwa na Zawadi Mwambi wa Pwani aliyetumia saa 1:06:12 na Joanita Alistides wa Zingiziwa aliyetumia dakika 1:07:22.
Huku kwa zile mbio za kilometa 5 wanaume washindi ni Felix Magoti wa Parokia Chuo aliyetumia dakika 20:40:05, akifuatiwa na Benedictor Tungaraza wa Parokia Chuo na Justin Shirima aliyetumia dakika 21:57:56.
Wakati kwa wanawake washindi ni Veneranda Paul wa Kibwegere aliyetumia dakika 32:47:15, akifuatiwa na Evarista Kimaro wa Msakuzi aliyetumia dakika 32:49:06 na Restusta Mtangira wa Magomeni aliyetumia dakika 35:26:08.
