Songea-Ruvuma.
Furaha na ahueni imerejea kwa mamia ya wakazi wa Manispaa ya Songea, baada ya kurejeshewa huduma ya maji kufuatia ofa ya msamaha wa faini iliyotolewa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Kupitia ofa hiyo iliyoanza Mei 8 hadi Mei 31, 2025, wananchi waliokuwa wamekatiwa huduma ya maji kutokana na madeni walipewa nafasi ya kulipa bila kutozwa faini, na kuweka makubaliano ya kulipa madeni yao kwa awamu, tangu kuanza kwa ofa hiyo wateja 287 wameitikia mwito huo, wamelipa zaidi ya Shilingi milioni 15, na tayari wameanza kufurahia huduma ya maji safi majumbani mwao.
“Nilikuwa nimekatwa maji kwa zaidi ya miezi mitatu, lakini baada ya kusikia kuhusu ofa ya Rais Samia, nilienda SOUWASA na walinisikiliza vizuri. Wakanirudishia maji bila faini, na sasa ninalipa kidogo kidogo. Naishukuru serikali,” alisema Bi. Mariam, mkazi wa Mshangano.
“Mwanzoni niliogopa kwenda ofisini kwa sababu nilidhani nitalazimika kulipa kila kitu papo hapo, lakini walikuwa na utaratibu mzuri, wamenisaidia na sasa nimeanza kulipa polepole,” alieleza Bw. Julius Komba, mkazi wa Bombambili.
Kwa mujibu wa Baby Lucas Biko, Mkurugenzi wa Huduma kwa Wateja wa Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira Songea (SOUWASA), ofa hiyo imeleta nafuu kwa wakazi wengi waliokuwa wakiteseka kutokana na kukatiwa huduma.
Amesema kabla ya ofa, zaidi ya wateja 2,400 walikuwa wamesitishiwa huduma ya maji, lakini sasa wengi wanaendelea kurejeshewa huduma kupitia makubaliano maalum ya ulipaji wa madeni.
Biko amewahimiza wateja wengine waliopitwa na ofa kuendelea kujitokeza, kwani SOUWASA bado inawakaribisha kwa mazungumzo ili kupata suluhisho la pamoja, amewakumbusha kuwa kulipa bili kwa wakati ni njia bora ya kuepuka usumbufu wa kukatiwa huduma na gharama za ziada.
Kwa wananchi wa Songea, ofa hii imekuwa zaidi ya msamaha imekuwa mkombozi kwa maisha ya kila siku, hasa kwa familia ambazo zilikuwa na changamoto ya kifedha kulipia madeni kwa wakati mmoja pamoja na faini hivyo wamepata fursa yakulipia kwa awamu na kurejeshewa huduma hii muhimu na hitaji la msingi la kila siku.