Katika kuadhimisha Siku ya Mazingira Duniani mwaka 2025, Shirika lisilo la Kiserikali Agenda for Environment and Responsible Development limeitaka jamii kuongeza juhudi za kupunguza matumizi ya Plastiki nchini.
Akizungumza leo Juni 4, 2025 katika hafla ya Maadhimisho ya Siku ya Mazingira Duniani, Katibu Mtendaji wa AGENDA Bi. Dorah Swai, amesema kuwa jamii ina wajibu wa kushiriki katika kupunguza matumizi ya Plastiki ili kulinda mazingira.
Bi. Swai amesema kuwa mwaka 2023 Tanzania ilizalisha tani zaidi ya 350,000 za taka za Plastiki, huku akieleza kuwa chini ya asilimia 10 ndizo zilizorejelezwa na nyengine kuishia katika uchafuzi mazingira.
“Taka za Plastiki hukaa ardhini kwa miaka 400-1,000 na ni hatari kwa viumbe hai kama binadamu, mimea, wanyama wa nchini kavu na majini kama samaki, hivyo tunapaswa kuchukua hatua” amesema Bi. Swai.
Makamu Mwenyekiti wa Bodi ya AGENDA Dkt. Zainab Katima, amesema kuwa wakati umefika kwa jamii kuendelea kuchukua hatua mbalimbali zikiwemo kupunguza matumizi ya plastiki zinazotumika mara kwa mara kama chupa, vifungashio pamoja na kutenganisha taka zinazoweza kurejelezwa na zile zisizoweza.
“Tunapaswa kutumia bidhaa mbadala kama mifuko ya kitambaa au vikapu vya asili pamoja na kuendelea kutoa elimu kuhusu madhara plastiki kwa mazingira na afya ili kulinda kizazi cha sasa na kijacho” amesema Dkt. Katima
Afisa Programu Mkuu wa AGENDA Bw. Silvani Mng’anya, amesema kuwa vitendo vinavyochangia uchafuzi wa mazingira ni pamoja na kutupa ovyo plastiki zinazotumiwa mara moja, kuchoma taka za Plastiki, kupika chakula kikiwa ndani ya plastiki pamoja na kubeba chakula katika mifuko ya plastiki.
Bw. Mng’anya ametaja baadhi athari zitokanazo na plastiki kuwa kuathiri mifuko ikolojia ya bahari, kuchafua mazingira kutokana inakaa muda mrefu bila kuoza pamoja na kuharibu miundombinu kwa kuziba mifereji na baadhi ya njia za maji.
“Natoa wito kwa Serikali kusimama imara katika majadiliano yanayoendelea ya kuwa na mkataba wa kimataifa wa plastiki ili kuhakikisha unakuwa shirikishi Kwa wadau wote zikiwemo asasi za kiraia” amesema Bw. Mng’anya.
Kila mwaka Juni 5 Duniani inaadhimisha Siku ya Mazingira ambapo mwaka huu imebaba kauli mbiu isemayo: Punguza uchafuzi wa Mazingira Unaochangiwa na Plastiki.