Mkuu wa Wiliya ya Ukerewe, Mheshimiwa Christopher Emily Ngubiagai amewashukuru wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwa kukarabati madarasa mawili na madawati 200 kwa ajili ya Shule ya Msingi Hamkoko.
Akipokea msaada huo kutoka kwa Mkurugenzi wa Rasilimali Watu wa Benki ya CRDB, Godfrey Rutasingwa, mkuu huyo wa wilaya amesea mazingira mabovu ya madarasa yanasababisha utoro kwa watoto wengi jambo ambalo seriklai inashirikiana na wadau kulifanyia kazi ili watoto wote wasome kwa utulivu unaohitajika kufanikisha ndoto zao.
“Hakika leo wafanyakazi wa Benki ya CRDB mmetupa somo kwa kujitoa kwenu kuhakikisha mnaigusa jamii jamii yetu ya wana Ukerewe. Hakika huu ni upendo mkubwa sana kutoka kwa wafanyakazi ambao sio tu inatugusa jamii ya hapa Ukerewe bali Tanzania nzima kwa ujumla. Mmeonyesha kujali na alama hii ya upendo haitosahaulika. Asanteni sana kwa heshima hii kubwa mliyotupa,” amesema Mheshimiwa Ngubiagai.
Amesisitiza kuwa shule zikiwa na miundombinu mizuri huwafanya watoto wapende kusoma kutokana na kuvutiwa na mazingira mazuri na madarasa ya kisasa, madawati bora ya kukalia. Kwa kulitambua hilo, amesema serikali inafanya kila liwezekanalo kuhakikisha inajenga shule mpya popote inapohitajika nchini na kukarabati miundombinu ya hsule za miaka mingi.
Akizungumza na wazazi, walimu na wanafunzi waliokuwepo kwenye hafla ya kukabidhi madarasa na madawati hayo, Mheshimiwa Ngubiagai amesema ni muhimu kwa jamii kujitoa kuchangia kuboresha mazingira ya shule kwa ajili ya watoto wa Kitanzania kujifunza kwa umakini na akaitumia nafasi hiyo kuwapongeza wafanyakazi wa Benki ya CRDB kwa kuonyesha mfano katika kujitoa kwa jamii wanaoyoihudumia na inayowazunguka.
“Hii imekuwa bahati kwetu kwani mngeweza kwenda sehemu nyingine lakini mliona inafaa kuja Ukerewe kusaidia kutatua changamoto za madarasa na kutoa madawati haya 200. Kwa kweli mmetufundisha na kutupa deni kubwa mioyoni mwetu kwani Watanzania wengi huwa wepesi kuchangia harusi na sherehe nyingine ila wazito kujitoa kwenye elimu kama mlivyofanya wafanyakazi wa Benki ya CRDB,” amesema.
Kwa upande wake, Rutasingwa amesema msaada huo umetolewa kupitia Programu ya Employee Volunteering iliyoanzishwa mwaka 2020 ambapo wafanyakazi wa Benki ya CRDB huchanga fedha kutoka kwenye mishahara yao na kuielekeza kutatua kero iliyopo kwenye jamii katika sekta ya elimu, afya, mazingira na watu waishio katika mazingira magumu.
“Moyo huu wa kujitoa kwa wafanyakazi wetu ni mwendelezo wa jitihada zinazofanywa na Benki ya CRDB kurudisha na kuwekeza katika jamii inapotoa huduma. Benki yetu hutenga asilimia moja ya faida yake baada ya kodi kwa ajili ya kuiwezesha jamii. Tunachangia madarasa, madawati, na miundombinu mingine ya shule. tunatoa vifaatiba na kuhamasisha afya ya jamii. Kupitia kampeni ya Pendezesha Tanzania, tunashiriki kutunza mazingira ili kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na tupo mstari wa mbele katika kuwawezesha wanawake na vijana kujitegemea kiuchumi,” amesema Rutasingwa.
Mkurugenzi huyo amefafanua kuwa utekelezaji wa Programu ya Employee Volunterring unaanzia ngazi ya mfanyakazi mmoja mmoja, matawi, ofisi za kanda mpaka idara za makao makuu ya Benki ya CRDB.
“Katika ngazi ya kanda, tayari tumeratibu na kutekeleza miradi katika kanda za Pwani, Dar es Salaam, na Kaskazini. Leo tunafungua ukurasa mpya wa jitihada hizi katika Kanda hii ya Ziwa kwa kukabidhi rasmi madarasa mawili na madawati 200 kwa shule hii ya Hamukoko hapa wilayani Ukerewe,” ameeleza Rutasingwa.
Kwa wazazi, Rutasingwa amewakumbusha umuhimu wa kuandaa mazingira haya ya kiuchumi kugharimia elimu akieleza kwamb benki ya CRDB inayo Akaunti ya Junior Jumbo inayomwezesha mzazi kuweka fedha taratibu kwa ajili y amahitaji ya mwanaye huku ikimwandaa mtoto kuwajibika kiuchumi kwa kuanza kutumia huduma za benki tangu akiwa mdogo.
“Akaunti hii haina makato na inamwezesha mzazi kuweka akiba kidogo kidogo kwa ajili ya masomo ya mtoto wake, kuanzia elimu ya awali hadi chuo kikuu. Unachohitaji ni cheti cha kuzaliwa cha mtoto, kitambulisho cha mzazi au mlezi, na shilingi 5,000 ya kuanzia ili kufungua akaunti hii,” amesema Rutasingwa.