-Ahimiza mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita kutangazwa kwa wananchi
Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi, amevitaka vyombo vya habari vinavyomilikiwa na chama hicho kuzingatia weledi, hasa kuelekea Uchaguzi Mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Balozi Nchimbi amesema vyombo hivyo vina wajibu mkubwa wa kutumia weledi huo kutangaza mafanikio makubwa ya Serikali ya Awamu ya Sita, inayoongozwa na Mheshimiwa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Akizungumza Alhamisi, tarehe 5 Juni 2025, wakati wa kikao na baadhi ya wakuu wa idara wa vyombo vya habari vya CCM, wakiongozwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Uhuru Media Group (UMG), Dennis Msacky, Balozi Nchimbi alisisitiza kuwa weledi wa vyombo hivyo uendelee kuwa mfano wa kuigwa katika tasnia ya habari nchini.
Mazungumzo hayo yalifanyika katika Ofisi Ndogo za Makao Makuu ya CCM, Lumumba, jijini Dar es Salaam, ambapo pia aliwapongeza kwa namna wanavyoendelea kuwahabarisha wananchi kuhusu masuala yanayohusu Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
Balozi Nchimbi alisema vyombo hivyo vya habari, ambavyo ni sauti ya chama, vina jukumu la kuutangazia umma utekelezaji wa miradi mbalimbali ya kimkakati chini ya Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2020–2025, sambamba na kuanza kuchambua Ilani mpya ya chama hicho kwa mwaka 2025–2030.
Kwa upande wao, wawakilishi wa vyombo hivyo walieleza namna walivyojipanga kufikisha taarifa kwa jamii, zikiwemo elimu ya uraia kuelekea uchaguzi, namna ya kushiriki, na mchakato wa kuwapata wagombea bora ndani ya CCM, kwa lengo la kuhakikisha chama hicho kinapata ushindi wa kishindo.