NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
CHUO Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) kinatarajia kufanya maadhimisho ya Wiki ya 10 ya Utafiti na Ubunifu (RIW)kuanzia Juni 9 hadi Juni 11 mwaka huu katika Viwanja vya Maktaba Mpya,Kampasi ya Mwalimu Julius Nyerere Mlimani.
Akizungumza leo Juni 5,2025 jijini Dar es Salaam Naibu Makamu wa Chuo-Utafiti katika Chuo hicho Profesa Nelson Boniface amesema sherehe ya ufunguzi wa maadhimisho hayo yatanyika Juni 9 mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Waziri wa Nchi,Ofisi ya Rais ,Mipango na Uwekezaji Profesa Kitila Mkumbo.
“Sherehe za kufunga maadhimisho yatafanyika Juni 11 mwaka huu na mgeni rasmi atakuwa Profesa Carolyne Nombo ambaye ni Katibu Mkuu Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia.Kauli mbiu itakuwa inasema “Kutumia Teknolojia ya Kidijitali ili kuharakisha Utafiti,ubunifu na ubiasharishaji “
Amefafanua kuwa kauli mbiu hiyo ni kwa kuzingatia dhamira ya kimkakati ya kuteleza dira ya UDSM ya 2061 katika kuendeleza mabadiliko kupitia sayansi ,teknolojia na ubunifu kwa kuzingatia dira ya maendeleo ya Taifa 2050 kwa maendeleo endelevu na jumuishi ya kijamii.
Ameongeza kuwa Maadhimisho ya 10 yatajumuisha maonesho ya kazi za utafiti na ubunifu za wanafunzi na wafanyakazi, jumla ya miradi 104 itaoneshwa, pia kutakuwa na kongamano lenye mawasilisho ya mada mbalimbali zitakazoongozwa na Mada Kuu mbili:
Pia amesema Juni 11 wakati wa kuhitimisha wiki ya utafiti na ubunifu kutakuwa na utoaji wa tuzo kwa mtu mmoja mmoja na makundi yatakayofanya vizuri zaidi hivyo UDSM inawaalika kwa moyo mkunjufu wadau wote, watunga sera, viongozi wa sekta ya viwanda, washirika wa maendeleo, taasisi za elimu, na umma kwa ujumla kushiriki katika tukio hili la heshima.
“Wiki ya 10 ya Utafiti na bunifu ni jukwaa muhimu la kuimarisha juhudi za kitaifa kuelekea tungaji wa sera kwa kuzingatia data za kitafiti, maendeleo yanayozingatia mabadiliko ya teknolojia, na ustawi jumuishi. Chuo Kikuu cha Dar es Salaam kinaendelea kuboresha nafasi yake ya kitaasisi kupitia viwango vya kimataifa vya vyuo vikuu na viashiria vya utendaji, na kinathibitisha tena dhamira yake.”