Na Mwandishi Wetu ,Dodoma
TAASISI ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) imetoa wito kwa wadau wa Kilimo kufanya shughuli za kilimo chenye tija ambacho kinazingatia uhifadhi wa Mazingira.
Wito huo umetolewa na Mtafiti Daines Sanga kutoka Kituo cha TARI Makutupora katika Maonesho ya wiki ya Mazingira yanayoendelea viwanja vya Ukumbi wa Jakaya Kikwete (JKCC) Jijini Dodoma kuanzia Juni 01-05, 2025.
Katika Maonesho hayo yenye kaulimbiu ya “Mazingira yetu na Tanzania ijayo Tuwajibike Sasa: Dhibiti Matumizi ya Plastiki” TARI inashiriki ikiwa na Teknolojia mbalimbali za Kilimo ambazo ni rafiki kwa Mazingira ikiwemo matuta ya kufunga maji, Teknolojia ya makinga Maji (Fanya juu/Fanya chini), kitalu Mkeka cha Mpunga pamoja na bidhaa zilizoongezeka thamani kutokana na Mazao mbalimbali ambazo ni Miongoni mwa Teknolojia Rafiki kwa Mazingira.
Akieleza kuhusu Teknolojia ya Matuta ya kufunga maji, Bi. Sanga amesema inasaidia kutunza maji kwa muda mrefu hususani maeneo ambayo mvua huwa ni chache na maeneo hayo yanategemea Kilimo cha Mvua.
Ametaja faida zingine kuwa ni kusaidia kuvuna maji ya mvua na kuhifadhi unyevunyevu shambani.
Kuhusu Teknolojia ya Kinga Maji Maarufu kama Fanya chini/ juu Mtafiti amesema inasaidia kuhifadhi Mazingira kwani inazuia mmomonyoko wa Udongo, inazuia upotevu wa rutuba ya Udongo, inavuna maji ya mvua shambani ambayo Mkulima anaweza kuyatumia katika shughuli za kilimo na inahifadhi unyevu shambani.