Na MWANDISHI WETU
MKURUGENZI Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji Raymond Mndolwa, amefanya ziara ya kushtukiza na kukagua mradi wa Umwagiliaji Mkoani Simiyu ukiwemo mradi wa ujenzi wa bwawa la Umwagiliaji na skimu ya Kasoli, iliyopo Kata ya Kasoli Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu na kutoa maelekezo kwa watendaji na mkandarasi ikiwemo kuzingatia viwango vya ubora wa ujenzi huo.
Akizungumza katika ziara hiyo ya ghafla mkoani humo Mndolwa, amesisitiza kuwa Serikali inatumia zaidi ya shilingi bilioni 8.021 kama thamani ya mradi huo, hivyo hatakubali kuona utekelezaji wake ukiwa wa kusua sua na viwango kuwa vya chini.
“Nataka kuona utekelezaji wa mradi unakuwa ndani ya muda tuliokubaliana lakini pia viwango vya ujenzi vizingatie ubora kulingana na thamani iliyopo,”alisema.
Mndolwa, alimtaka Mkandarasi anayetekeleza mradi huo Kampuni ya kigeni iitwayo SIETCO Jv JGC, kuongeza kasi ya utekelezaji wa ujenzi, kujenga barabara ya kuingia eneo la ujenzi na kuhakikisha ujenzi unafanyika kwa kiwango bora na kilichokusudiwa kwa kufuata matakwa ya mkataba..
Pia, alimtaka Mhandisi wa mkoa Jeramiah Seme, kushughulikia hati ya kiwanja iliyojengwa ofisi ya mradi huo.
Alisisitiza kuwa, bwawa hilo lililopo kijiji cha Kasoli, Kata ya Kasoli, Wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, lina ukubwa wa mita za ujazo milioni 2.7 3 na litahudumia mashamba yenye ukubwa wa hekta 650 .
Alisema, utekelezaji wa mradi umefikia asilimia 72.75.
Kwa upande wake Mhandisi wa Mkoa Seme, alieleza kuwa wamepokea maelekezo hayo na atahakikisha anasimamia ipasavyo ujenzi wa mradi huo ikiwemo kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Mkandarasi hususani katika suala la muda na viwango vya mradi.