Na Mwandishi Wetu,Morogoro
WAKATI kipyenga cha uchukuaji fomu kwa wagombea wa nafasi mbalimbali ikiwemo Urais, Ubunge na Udiwani kwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kwa ajili ya kuwapata wagombea wa kupeperusha bendera ya chama hicho kikiwa bado hata hakijapulizwa tayari michezo michafu ya inayohusishwa na rushwa imedaiwa kuanza katika jimbo la Uchaguzi la Morogoro Mjini.
Hatua hiyo imedaiwa kuwahusisha makatibu wa kata 27 kati ya 29 zilizopo katika jimbo hilo ambapo mchakato huo unadaiwa kufanywa kwa usaidizi wa Katibu wa CCM wa Wilaya ya Morogoro Mjini Twalib Bellege.
Kupitia kikao Cha Makatibu hao wa kata kilichoitishwa na Katibu wa Wilaya Juni 7, mwaka huu kikiwa na ajenda saba, pamoja na mambo mengine kilitoa maagizo kwa Makatibu hao kutumia nafasi walizonazo kumpigia Mbunge aliyepo sasa apite aweze katika kura za maoni na kugombea tena ubunge katika uchaguzi ujao.
” Tulipewa maagizo mbalimbali ambayo kimsingi mengine ya kiutendaji ikiwemo kuzingatia taratibu za ujazaji wa majina kwa kufuata alfabeti katika fomu za kuomba kuteuliwa ambayo tuliyapokea kama ilivyotakiwa.”
Alisema kikao hicho kilichofanyika katika Ofisi ya CCM Wilaya ya Morogoro Mjini, kiliwahusisha wajumbe kutoka Kata 27 kati ya Kata 29 zilizopo katika Wilaya hiyo Morogoro Mjini huku wakielezwa kuwa vikao vingine kama hivyo na vingine vya muendelezo wa mikakati hiyo vikipangwa kufanyika mbeleni.
” Tuliambiwa kuwa vikao hivyo ni vya siri na sote tulioidhuria hatupaswi kuvujisha siri hiyo kwa makubaliano maalumu, baada ya sisi na Katibu huyo wa Wilaya kukubaliana,”amedai na kuongeza wakiwa kikaoni zililetwa bahasha mbili moja kwa ajili yelao Makatibu wa Wilaya na bahasha nyingine kwa ajili ya viongozi wa Wilaya.
” Kwa sisi tunaopenda haki na kuepuka kukichafua Chama chetu ambacho kimejipambanua kusimamia haki kwa kila mgombea jambo hili hatukuliona kama linapaswa kufumbiwa macho lakini huwezi kusema mbele ya wajumbe wenzako kwa kuwa ungeonekana kuwa msaliti” ameongeza mtoa taarifa huyo ambaye jina lake limehifadhiwa
Amedai hiyo sio mara ya kwanza kufanyika rafu za kisiasa katika wilaya hiyo chini ya Katibu huyo wa Wilaya kwani hapo awali aliwahi kuitisha kikao cha haraka haraka cha wenyeviti wa Serikali za Mitaa kwa kisingizio kuwa ni semina, ilipojulikana kuwa wevyeviti na Mabalozi watapiga kura za maoni ndani ya Chama.
Kwa upande wake Mjumbe mwingine ambaye kama alivyo kwa Mjumbe wa kwanza amedai kuwa mtengenezaji wa mazingira yote hayo ni Katibu wa CCM Wilaya.
Aidha ameziomba mamlaka ambazo zinahusika na uchunguzi kuifanyia kazi suala hilo kwa madai kuwa kama halitoshughulikiwa linaweza kubaribu mchakato wa uchaguzi unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.
Akijibu tuhuma hizo Katibu huyo wa CCM Wilaya ya Morogoro Twalib Berege alikana kugawa fedha hizo kwa wajumbe hao huku akisisitiza kuwa kwa Kipindi hiki tuhuma na malalamiko kama hayo ni kawaida kutokea.
“Ajenda ya kikao ilikuwa moja tu kuhusu maandalizi ya Uchaguzi, huyo aliyesema kuwa tuligawa fedha basi akuthibitishie lakini hata kama kweli huyo anayetajwa kutoa fedha angefanya hivyo ndani ya Chama haina tatizo kwa kuwa yupo madarakani anakisaidia Chama”
“Kwanza Mbunge mwenyewe kwa sasa yupo nje ya nchi, angewezaje kuja katika kikao na kutoa fedha hizo” alisema Katibu huyo na hata alipoambiwa kuwa aliyetumwa kuleta fedha hizo ni ndugu wa Mbunge huyo alisisitiza kuwa hakuna kitu kama hicho.
Alipotafutwa Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya hiyo ya Morogoro ili kupata ufafanuzi wa suala hilo, aligoma kutoa ushirikiano akidai kutokuwa na taarifa yoyote juu ya kufanyika kwa kikao hicho na badala yake akashauri atafutwe Katibu Mwenyewe.