Dar es Salaam, Juni 10, 2025 – Airtel Tanzania imeibuka nafasi ya pili katika mashirika yaliyotoa gawio kubwa kwa serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa mwaka wa fedha 2024/25, na kuwasilisha hundi ya Shilingi bilioni 73.9 kwenye hafla ya siku ya Gawio iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam. Hafla hiyo iliandaliwa Ofisi ya Msajili wa Hazin na kuhudhuriwa na Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Utoaji wa Gawio na Mchango huo sio tu inadhihirisha ufanisi na kukuaji kwa Airtel kibiashra bali unaonyesha jinsi Airtel ilivyojidhatiti kuendelea kuwa mdau muhimu wa maendeleo ya taifa kupitia ushirikiano wa kimkakati baina ya sekta ya umma na sekta binafsi.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alitoa shukrani kwa mashirika ya sekta binafsi kwa kuchangia kiasi cha trilioni 1.28 kwa mwaka huu. Pia alisisitiza kuwa Serikali inaendelea kuweka mazingira bora ili kuendelea kuchochea uwekezaji na kuongeza kasi ya ukuaji kiuchumi.
Mhe. Rais Dkt Samia Suluhu hassan ameeleza kuwa siku ya hiyo inadhihirisha muelekeo wa serikali katika uendeshaji wa mashirika ya umma huku akiyataka yaweze kuzalisha na kujiendesha yenyewe.
“Nawapongeza wote ambao mmeweza kuchangia. Siku hii inatoa fursa kwa wananchi kuona namna mashirika mbalimbali yanawajibika kwao. Niyatake mashirika na taasisi kuongeza ubunifu kwa lengo la kuongeza ufanisi katika utendaji na kutatua changamoto zinazowakabili,” alisema Dkt Samia.
Pia Mheshimiwa Rais Dkt. Samia alitoa rai kwa mashirika ambayo yanamilikiwa na serikali kwa hisa yahakikishe yanatumia kikamilifu mifumo ya TEHAMA ili kuongeza ufanisi na tija na uwazi katika utendaji.
Tangu mwaka 2019, Airtel Tanzania Plc pamoja na Airtel Money Tanzania Ltd zimechangia jumla ya zaidi ya shilingi bilioni 280 kwa serikali. Kupitia umiliki wa serikali kwa asilimia 49, kampuni hii imebaki kuwa mfano wa namna ushirikiano na sekta binafsi unaweza kuleta manufaa ya muda mrefu.
Akizungumza baada ya makabidhiano hayo, Mwenyekiti wa Bodi ya Airtel Tanzania, Eliudi Sanga, alibainisha kuwa kujituma kwa Airtel kuna mchango mkubwa katika kuchochea mabadiliko ya kiuchumi na kijamii.
“Airtel Tanzania inajivunia kuwa mshirika wa kuaminika katika safari ya maendeleo ya taifa. Uwekezaji wetu unaendana na vipaumbele vya kitaifa vya Serikali kwa kupanua miundombinu ya kidijitali kwa kuchangia upatikanaji uliojumuishi na wezeshi wa uchumi wa kidijitali,” alisema Sanga.
Kwa upande wake, Charles Kamoto, Mkurugenzi Mtendaji wa Airtel Tanzania, alisisitiza juu ya malengo ya kampuni kuwezesha ukuaji jumuishi na uwezeshwaji wa kidijitali.
“Mchango wa gawio letu ni kielelezo cha msimamo wetu katika kuchagiza kwenye maendeleo endelevu ya Tanzania. Hii inaakisi namna sera ya serikali inavyoendana na ubunifu wa sekta binafsi katika kuleta maendeleo jumuishi na kuelekea katika uchumi wa kidigitali,” alisema Kamoto.
Kamoto alihitimisha kwa kusema kuwa Airtel inajivunia kuiunga mkono serikali kupitia uwekezaji wake kupitia upanuzi wa mtandao, unafuu wa vifaa vya mawasiliano na majukwaa ya kidijitali nchini Tanzania.