📍NIRC; Dodoma
Serikali ya Awamu ya Sita, kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, imeanza utekelezaji wa ahadi ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ya uchimbaji wa visima virefu 67,000 vya maji kwa ajili ya kiliko cha Umwagiliaji nchini.
Lengo ni kuhakikisha kuwa Taifa linaondokana na kilimo cha kutegemea mvua na kuwa na uhakika wa maji kwa ajili ya kilimo na kulima zaidi ya mara moja kwa mwaka
Hatua hiyo imetokana na ahadi ya Rais Dkt.Samia, aliyoitoa wakati wa maazimisho ya siku ya Wakulima Duniani( Nane Nane), yaliyofanyika kitaifa jijini Mbeya, mwaka 2023.
Hayo yamesemwa leo jijini Dodoma na Mkurugenzi Mkuu Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC), Bwana Raymond Mndolwa, wakati wa kuanza kwa zoezi la uchimbaji wa visima kwa kutumia mitambo iliyonunuliwa na Serikali katika mashamba ya BBT (Chinangali) ya programu ya Jenga Kesho iliyo Bora (BBT), inayowawezesha vijana kujiajiri katika kilimo.
Mndolwa amesema Serikali ya Dr. Samia imeiwezesha Tume kununua mitambo ya kisasa ya kuchimba visima virefu, lengo likiwa ni kuhakikisha kunakuwa na mazingira wezeshi ya upatikanaji wa maji kwa ajili ya kiliimo cha Umwagiliaji na Taifa linaondokana na kilimo cha msimu mmoja na kulima mara mbili au zaidi.
“Tume imenunua mitambo 17 ya kuchimba visima kwa thamani ya shilingi bilioni 17.5 yenye uwezo wa kuchimba mita 300 hadi 1,800, ambapo mitambo 7 inachimba visima katika shamba hili la Chinangali na tunashuhudia visima vikiwa na maji ya kutosha kabisa.
“Miundombinu yote ya Umwagiliaji katika shamba hili ipo tayari na sasa hatua inayofuata ni kuhakikisha maji yanapatikana kwa kuchimba visima 29 hapa na visima vingine 40 vitachimbwa katika shamba la BBT (Ndogowe) ili vijana waliopata mashamba haya walime kwa uhakika. Tume ya Taifa ya Umwagiliaji kwa nguvu mpya, imejidhatiti kutimiza jukumu hilo muhimu”, amesema.
Mndolwa amesema, dhamira hiyo haishii Chinangali na Ndogowe pekee na kwamba Mpango wa uchimbaji visima unatarajiwa kutekelezwa nchi nzima na kuhakikisha kuwa siyo vijana tu, bali wakulima wa kada zote wanapata maji ya uhakika kwa kilimo endelevu.
“Mitambo hii itapita mkoa kwa mkoa, wakulima wajiandae kuchangamkia fursa hii wakiwa katika makundi ya wakulima zaidi ya 16 na ekari kuanzia 40 ili waweze kupata kisima”
Mndolwa ameongeza kuwa Serikali ya Dr. Samia imedhamiria kwa dhati kubwa kumwinua mkulima wa Tanzania ambapo miaka minne iliyopita, miradi ya umwagiliaji ilikuwa 13 pekee, lakini leo hii idadi imeongezeka hadi kufikia miradi 780 pamoja na mpango huu wa visima 67,000 nchi nzima.