Na Farida Mangube, Morogoro
Kampeni ya kitaifa ya msaada wa kisheria ya Mama Samia imewasaidia wafungwa na maabusu zaidi ya 12,000 katika magereza nchini, ambapo kati yao maabusu 6,900 wametolewa huru baada ya kupata msaada wa kisheria.
Kamishna wa Sheria na Uendeshaji wa Magereza, CP Nicodemus Tenga, alisema hayo wakati wa ufunguzi wa mafunzo ya awamu ya pili ya kuwajengea uwezo maafisa sheria na urekebu wa Jeshi la Magereza kuhusu huduma za msaada wa kisheria, mapokezi ya wafungwa magerezani, na utekelezaji wa adhabu mbadala.
CP Tenga alisema idadi ya wafungwa katika magereza imepungua kutoka zaidi ya 32,000 mwaka 2021 hadi kufikia 26,896 Juni 9, 2025. Alibainisha kuwa uwiano wa wafungwa na maabusu umebadilika kutoka nusu kwa nusu hadi sasa wafungwa kuchangia asilimia 75 na maabusu asilimia 25.
“Kwa sasa uwezo wa magereza ni wafungwa 29,102 lakini tunaupungufu wa zaidi ya wafungwa 3,000, hivyo kuna nafasi katika magereza,” alisema CP Tenga.
Alifafanua kuwa Jeshi la Magereza lina vituo 129, ikiwemo vituo 26 vya mikoa na vituo vingine vya vikosi pamoja na shule sita za magereza. Hata hivyo, wilaya 50 bado hazina magereza, na wafungwa kutoka wilaya hizo hufikishwa magerezani wilaya jirani, akitoa mfano wa wilaya za Kakonko na Uvinza.
Mkurugenzi wa Katiba na Ufuatiliaji Haki kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Jane Lyimo, alisema mafunzo hayo yanalenga kuongezea uelewa wa haki za binadamu, usimamizi wa haki za wafungwa, utekelezaji wa adhabu mbadala na usimamizi wa mikataba ya magereza.
“Tunatarajia kuzingatia haki za binadamu, kujenga mfumo wa haki unaotenda kazi kwa ufanisi, uwazi na kutumia ushahidi wa kisheria,” alisema Lyimo.
Mafunzo hayo kwa awamu zote mbili yaliwashirikisha washiriki 290 kutoka mikoa yote nchini, na ni sehemu ya juhudi za serikali kuimarisha mnyororo wa haki jinai nchini.
Naibu Katibu Wizara ya Katiba na Sheria, Franklin Rwezimula, akizungumza kwa niaba ya Katibu Mkuu Wizara hiyo wakati akifungua mafunzo hayao aliwatahadharisha maafisa wa magereza kuhusu jukumu kubwa la kusimamia hatua ya mwisho ya mnyororo wa haki jinai. Alisema jukumu hilo linahitaji ujuzi wa kitaalamu, uadilifu, uelewa wa sheria na mbinu za urekebu wa tabia.
“Katika dunia yenye mabadiliko ya kasi hususan katika nyanja za usalama, kijamii na kisheria, ni wajibu wa Jeshi la Magereza na Taifa kuwekeza kwa makusudi katika uimarishaji wa uwezo wa watumishi wa umma,” alisema Rwezimula.