Na Said Mwishehe, Tunduru
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Stephen Wasira, amewataka Watanzania wakiwemo wanachama na wapenzi wa Chama hicho kujiandaa kwenda ‘kutiki’ kwa kumpigia kura Mgombea Urais wa CCM, Dk. Samia Suluhu.
Amesisitiza hakuna mtu au kikundi cha kuzuia uchaguzi huku akiwataka wananchi kutobabaishwa na kaulimbiu ya ‘No Reform No Election’ ya CHADEMA kwa kuwa inakwenda mwishoni kwa kuwa tayari CCM na wanachama wake wamejiandaa kutiki kwa Dk. Samia Oktoba mwaka huu.
Ameeleza hayo leo Juni 10, 2025 alipokuwa akizungumza na wana CCM, wananchi, viongozi wa dini na makundi mbalimbali ya kijamii katika kikao cha ndani wilayani Tunduru, Mkoa wa Ruvuma.
Wasira ametumia mkutano huo kueleza hatua kwa hatua sababu zinazoifanya CCM na Watanzania kumpigia kura Rais Dk. Samia Suluhu Hassan pamoja na mgombea mwenza wake Dk. Emmanuel Nchimbi ambaye pia ni Katibu Mkuu wa CCM.
“Usibabaishwe na maneno hakuna mtu wa kuzuia uchaguzi, utakuwepo na ninyi mabalozi toweni watu wetu waende wakapige kura muda ukifika, waende ‘wakatiki’ na tiki yenyewe ni rahisi maana unaona CCM na alama ya jembe na nyundo.
“…Utamuona mgombea wetu Dk. Samia Suluhu Hassan, utamuona Dk. Emmanuel Nchimbi halafu mbele ya hao watu unaweka tiki. Kwa hiyo nilitaka niwaeleze haya mambo muyajue vizuri ili msije kubabaishwa.” Alieleza.