Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
WAZIRI wa Madini, ambaye pia ni Mbunge wa Dodoma Mjini Anthony Mavunde amezindua Saccos ya Chama cha Madereva Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma (UMAPIDO) huku akiwataka kujiunga kwa wingi ili kuongeza mtaji wa chama hicho.
Akizungumza katika uzinduzi huo uliofanyika katika ofisi za Chama hicho Makole Jijini hapa,Mavunde alimshukuru Rais Samia kwa kuendelea kuwajali maafisa usafirishaji.
Amesema dhamira yake ni kuona umoja huo unazidi kusonga mbele ikiwa ni pamoja na bodaboda kuweza kumiliki bodaboda zao wenyewe ili kujiongezea kipato.
“Naomba nitoe rai kwa wale ambao sio wanachama kuitumia fursa hii ya kujiunga lengo tunataka muendeshe bodaboda zenu na lengo sio kausha damu bali kuwaongezea damu na hili mimi nitalisimamia kwa nguvu zangu zote nataka kuwainua kiuchumi”alisema Mavunde.
Katika hatua nyingine Mavunde alimeliomba Jeshi la Polisi pamoja na Latra kuwa karibu na bodaboda ili waweze kufanya kazi zao vizuri na kuwacha kuwakamata bila sababu za msingi.
“Nawaomba Polisi muwafanye hawa wawe marafiki zenu natamani kuona Afisa usafirishaji akimuona askari asimkimbie amuone rafiki yake,”alisema Mavunde na kushangiliwa na bodaboda hao.
Kwa upande wake Yahya Kiyabo ambaye ni Mkuu wa Idara wa Biashara na Ushirika toka benki ya Ushirika Tanzania amesema kupitia benki hiyo kuna fursa mbalimbali wamewapatia bodaboda.
Amezitaja fursa hizo kuwa pamoja na huduma ya kufungua akaunti ambapo kuna akaunti maalumu kwa bodaboda kwa kulipa Sh 5000 na anapewa zawadi ya T-shirt na lita tatu za mafuta.
Alisema anaefungua akaunti ikitokea umefariki wanatoa mkono wa pole uziopungua Sh milioni moja, na huduma ya bima kubwa na ndogo.
“Tumekubaliana kuwapatia bima ya afya na mchakato unaendelea lengo ni kuhakikisha Afisa usafirishaji anafanya kazi yake bila changamoto yoyote,”alisema Kiyabo.
Naye,Mkuu wa Wilaya ya Dodoma,Jabir Shekimweri amewapongeza maafisa usafirishaji kwa kuweza kusajili Saccos yao ambapo ameahidi kuwapa ushirikiano na Umoja na mshikamano ndio utakawavusha.
“Naiomba bank ya Ushirika kuweni karibu na hii benki kwani kwenye fedha kadhia nyingi huwa zinajitokeza,niwaombe muwapatie mafunzo na wataelewa na itakuwa ya mfano,”alisema Shekimweri.
Hata hivyo,Shekimweri aliwataka Madereva wa bodaboda na Bajaji kuwa makini kwenye uendeshaji wao kwa kuyapenda maisha yao na kuchukua tahadhari.
Naye,Kamanda wa Polisi Mkoa wa Dodoma,George Katabazi aliwataka bodaboda kutii sheria bila shuruti ambapo amedai hakuna sababu ya kuanza kukimbizana kwani wote ni ndugu.
“Nawaomba mtoe taarifa za uhalifu na wahalifu,msijihusishe na uhalifu,tuendelee kudumisha amani tuache kufanya vurugu,”alisema Kamanda Katabazi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Bodaboda na Bajaji Mkoa wa Dodoma (UMAPIDO), Chacha Marwa amesimulia jinsi mikopo umiza, kaushadamu ilivyosababisha waanzishe Chama cha Kuweka na Kukopoa (Sacoss).
Marwa amesema wazo la kuanza kwa chama hicho lilianza tangu mwaka 2017.
“Tumenuia kwamba mikopo ilikuwa inatuumiza, inaitwa kausha damu. Mheshimiwa mgeni rasmi nikwambie hakuna watu wanakopa kama maofisa usafirishaji (bodaboda) na kausha damu inatutesa kweli,”amesema.
“Unakopa laki moja unarudisha laki tatu hivi kweli ni haki. Mimi nikasema siwezi kuongoza chama cha namna hii, watu wanamalizwa na kausha damu. Nikasema tunaweza tukaanzisha Saccos,”amesema.
Amesema waliamua kuanza na kidogo walicho nacho na leo hii wanazindua wakiwa na zaidi ya Sh11 milioni.
Amesema mikopo hiyo itawapa nafasi waendesha bodaboda hao kununua pikipiki na bajaji zao wenyewe badala ya kuendesha za watu.
Awali akisoma risala ya Umoja huo,Katibu wa Umojaà huo,Sarah Kiyando alisema wana malengo ya kutoa mikopo nafuu ili kuwaokoa bodaboda na mikopo ya kausha damu,kuondoa masharti magumu katika mikopo,kuhakikisha wanapata bima.