Tunduru-Ruvuma.
Mnada wa pili wa zao la ufuta kwa msimu huu umefanyika leo tarehe 11 Juni 2025, ambapo jumla ya kilo 1,570,146 za ufuta zimeuzwa kwa bei ya juu ya shilingi 2,420 kwa kilo huku bei ya chini ikiwa shilingi 2,410, bei ya wastani katika mnada huu ilikuwa shilingi 2,413 kwa kilo.
Akizungumza mara baada ya kukamilika kwa mnada huo, Afisa Ushirika kutoka Tume ya Maendeleo ya Ushirika Tanzania, tawi la Tunduru, Raymond Rafael alieleza kuwa mnada huu ulianza rasmi jana tarehe 10 Juni 2025 katika kata ya Mtina, kijiji cha Muungano.
Afisa Rafael amebainisha kuwa kumekuwa na kushuka kwa bei ya wastani kwa shilingi 26 ukilinganisha na mnada wa kwanza ambapo bei ya wastani ilikuwa shilingi 2,439 kwa kilo.
Amefafanua kuwa mabadiliko haya yanatokana na mwelekeo wa soko la dunia pamoja na viwango vya ubora wa ufuta unaozalishwa, amesisitiza umuhimu wa wakulima kuzingatia usafi na ubora wa mazao yao ili kuweza kuhimili ushindani kwenye soko la kimataifa.
Kwa upande wake, Kaimu Meneja wa Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru (TAMCU Ltd.), Ndugu Yasini Masyano, amesema kuwa tayari malipo ya mnada wa kwanza yameanza kufanyika na kiasi cha zaidi shilingi bilioni 3.7 kimekwishalipwa kwa wakulima husika.
Baadhi ya wakulima waliopata fursa ya kuzungumza kwa nyakati tofauti wameishukuru serikali kwa kuhakikisha wanalipwa kwa wakati fedha zao za mnada wa kwanza, hata hivyo waliomba serikali kuendelea kufuatilia kwa karibu mwenendo wa soko la dunia ili kusaidia kudhibiti kuporomoka kwa bei za mazao yao.
Mnada huu wa pili unaonesha changamoto na mafanikio kwa wakati mmoja, huku viongozi wakisisitiza ushirikiano kati ya wakulima, vyama vya ushirika, na serikali katika kuhakikisha sekta ya kilimo inakuwa na tija zaidi kwa mkulima wa kawaida.