Na Mwandishi wa NCAA, Ngorongoro
Waongoza utalii kutoka kampuni mbalimbali zinazojihusisha na shughuli za utalii nchini wameipongeza uongozi wa Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro (NCAA) kwa juhudi wanazofanya kuboresha miundombinu ya barabara katika Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro.
Wadau hao wameelezeq hatua hiyo kuwa ni suluhisho la muda mrefu kwa changamoto zilizokuwa zikiwakabili, hasa wakati wa msimu wa kilele cha utalii (high season)
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika geti la kuingia hifadhi ya Ngorongoro Juni 11, 2025, baadhi waongoza utalii hao wameeleza kuwa maboresho hayo yameleta mabadiliko makubwa katika usafiri, kupunguza muda wa safari, kuongeza usalama wa wageni, na kuboresha hali ya utalii katika hifadhi hiyo maarufu duniani.
“Tunatoa pongezi kwa NCAA kwa kazi kubwa waliyoifanya kuboresha barabara, kwa sasa imekuwa rahisi zaidi kuwafikisha wageni kwa haraka na salama kwenye maeneo ya vivutio vya utalii vilivyopo Ngorongoro” alisema Mohammed Tenga kutoka kumpuni ya Zara Tours.
Kwa upande wake Walter Temba kutoka kampuni ya utalii ya Serengeti Smiles alieleza kuwa maboresho ya miundombinu ya barabara yanayoendelea yamekuja kwa wakati muafaka, ikizingatiwa kuwa sekta ya utalii nchini inaendelea kukua kwa kasi huku idadi ya wageni kutoka ndani na nje ya nchi ikiendelea kuongezeka kila mwaka.
“Kwa muda mrefu tumekuwa tukikumbana na changamoto kubwa hasa wakati wa mvua magari yanakwama na wageni kuharibika hata kabla ya kufika kwenye vivutio. Lakini sasa hali ni tofauti kabisa, barabara zimekarabatiwa kwa kiwango kizuri na zinaweza kupitika hata kipindi cha mvua ombi letu ni kuwa jitihada hizi ziwe endelevu,” alisema Temba.
Kwa Mujibu wa NCAA, maboresho ya barabara ni sehemu ya maandalizi ya taasisi hiyo kukabiliana na ongezeko kubwa la watalii ambalo limeanza mwezi juni ambalo linatarajiwa kuongezeka hadi mwezi Oktoba kila mwaka.
Eneo la Hifadhi ya Ngorongoro hupokea maelfu ya wageni kutoka mataifa mbalimbali duniani wanaokuja kutembelea vivutio vya utalii ambapo takwimu zinaonesha kuwa kati ya Mwezi Julai 2024 hadi Mei, 2025 jumla ya watalii 972,896 wametembelea hifadhi kwa shughuli za utalii.