Kassim Nyaki, Karatu Arusha.
Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii anayesimamia Maliasili CP. Benedict Wakulyamba amefunga mafunzo ya Afisa na Askari wa Jeshi la Uhifadhi NCAA yaliyofanyika katika kituo cha Mafunzo ya jeshi la Uhifadhi Mbulumbulu Wilaya ya Karatu Mkoani Arusha.
Akifunga mafunzo hayo yenye wahitimu 25 wanaojumuisha Naibu Kamishna mmoja (01), Makamishna Wasaidizi waandamizi wanne (04), Maafisa Uhifadhi wakuu kumi (10), Afisa Uhifadhi waandamizi watano (05), afisa uhifadhi daraja kwanza wawili (02), askari uhifadhi mkuu 01 na askari uhifadhi daraja la pili (02) CP. Kamishna Wakulyamba amewasisitiza wahitimu hao kuzingatia uwajibikaji katika Utumishi kwa kufuata taratibu, nidhamu ya kijeshi na kutumia vyeo walivyonavyo kama nyenzo ya utawala katika mfumo wa Kijeshi.
“Natumia fursa hii kuwapongeza wahitimu wote 25 kwa kuhitimu mafunzo haya muhimu ya mabadiliko ya utendaji, hakikisheni mnazingatia , maadili, uadilifu, ujasiri, uzalendo, nidhamu, uadilifu kuzingatia amri na nidhamu za kijeshi na kuongeza ubunifu katika usimamizi wa rasilimali za misitu na wanyamapori na kuhakikisha kuwa mnaendelea kupata mafunzo ya mara kwa mara na kutumika ipasavyo katika maeneo yenu” alisisitiza Wakulyamba
Akitoa taarifa kuhusu mafunzo hayo Mkuu wa Mafunzo hayo Kanali Fikiri Machibya ameeleza kuwa mafunzo kwa maafisa na askari hao yalijikita katika Uongozi wa kijeshi, Kwata, matumizi ya Silaha ndogo (SMG & PistoL, Itifaki na maadili, Ulinzi wa viongozi, General order (GO) na ulengaji shabaha
Akizungumza kwa niaba ya Kamishna wa Uhifadhi Naibu kamishna wa Uhifadhi NCAA, Joas Makwati ameeleza kuwa mafunzo yaliyotolewa kwa watumishi hao ni fursa kujifunza kwa nadharia na vitendo juu ya mabadiliko ya mfumo wa kiraia kwenda katika mfumo wa kijeshi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yamewabadilisha viongozi, maafisa na maaskari wa uhifadhi katika kuwajibikaji kwenye majukumu ya kila siku kwa kuzingatia misingi ya kijeshi, nidhamu na utiifu na kubainisha kuwa uongozi wa NCAA utaendelea kuendesha mafunzo ya mara kwa mara kwa maafisa na askari wa jeshi la uhifadhi.
Mratibu wa Jeshi la Uhifadhi kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii Kamishna Msaidizi Mwandamizi Fidelis Kapalata ameeleza kuwa Wizara hiyo inaendelea kuhakikisha kuwa watumishi wote wa taasisi za Uhifadhi zilizoko chini ya Wizara hiyo zinaendelea kupata mafunzo ya mara kwa mara ili kujiimarisha katika udhibiti wa vitendo vya ujangili na kuwa imara mda wote katika kuzilinda rasilimali za wanyamapori na misitu.