Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Waziri wa Kilimo Mhe Hussein Bashe amesema katika kuhakikisha wanalinda viwanda vya ndani Serikali imejipanga kununua mbolea tani laki 2 katika viwanda vya ndani na tani elfu 50 za chokaa kwaajili ya kuboresha shughuli za kilimo.
Waziri Bashe ameyasema hayo Jijini Dodoma Juni wakati akitoa taarifa juu ya Uzinduzi rasmi wa Kiwanda cha Mbolea cha Itracom Fertilisers Limited utakaofanyika Juni 28,2025 ambapo Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe Dkt Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuwa Mgeni rasmi.
Ambapo amesema ununuzi huo wa Mbolea hautalenga kuathiri mfumo wa ruzuku unaoendelea kwani wao watapeleka zaidi maeneo yale ambayo mbolea hazitumiki kwa wingi ili Watanzania wahamasike kuzitumia na kuona matokeo.
“Ili kulinda viwanda vyetu vya ndani Serikali mwaka huu imeamua itanunua mbolea kutoka viwanda vya ndani tani laki 2 na tani elfu 50 zitanunuliwa nu za chokaa kwaajili ya shughuli za kilimo”.
“Na pia Serikali itanunua hizi mbolea bila kuathiri mfumo wa ruzuku unaoendelea, ila zitakaponunuliwa tutazipeleka kwenye maeneo ambayo mbolea hazitumiki sana ili Watanzania waanze kutumia za viwanda vya ndani na kuona matoke yake”.
Aidha amesema Nchi imekuwa ikiagiza karibu tani milioni 1.2 za mbolea kutoka nje lakini kwasasa kutokana na uwepo wa kiwanda hiki na uwekezaji wake mahitaji ya mbolea yatapatikana kutoka viwanda vya ndani.
Naye Mkurugenzi wa Kiwanda cha Itracom Fertilisers Limited Bwana Nduwimana Nazaire amesema kuwa wao kwa kushirikiana na Taasisi za Serikali kama vile TARI na TFRA mpaka sasa tayari kuna aina 14 ambazo kiwanda kinazalisha ambapo pia kiwanda kina uwezo wa kutengeneza mbolea kulingana na eneo,kulingana na zao na pia kulingana na hitaji la mkulima.
Na kuongeza kuwa kiwanda hicho kinazalisha mbolea mchanganyiko wa chumvi chumvi na malighafi za asili kama vile samadi na zinginezo.
Uzinduzi huu ni miaka mitatu na nusu toka uwekezaji huu kuanza kufanyika hapa Jijini Dodoma.