Na Mwandishi Wetu,Songea
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Tanzania Bara, Stephen Wasira amesema uwepo wa demokrasia na uhuru wa kutoa maoni sio ruhusa ya kuvunja sheria, kutukana watu na kwamba anayefanya hivyo anastahili kuchukuliwa hatua ikiwemo kukamatwa na kuhojiwa polisi.
Amesema lengo la uhuru ni kutoa maoni na kufuata sheria ambazo zimewekwa kuifanya jamii iishi pamoja bila ya bughudha na kuondoa uwezekano wa mtu mmoja kumuonea mtu mwingine.
Wasira ameeleza hayo leo alipokuwa akizungumza na viongozi wa ngazi mbalimbali wa CCM wakiwemo mabalozi wa shina katika Jimbo la Peramiho, wilayani Songea mkoani Ruvuma.
“Siku hizi ukisoma mitandao eti matusi ndio demokrasia, eti matusi ndio uhuru ah! Uhuru wa kutukanana sasa hapo tumekosea njia, ungekuwa uhuru wenyewe ni wa kutukanana tungeutafuta wa nini, tulitafuta uhuru ili utusaidie kujenga watu pamoja kuleta amani katika nchi na kusimamia maendeleo yao.
“Uhuru ni kutoa maoni, uhuru ni kufuata sheria maana unaweka sheria ambazo zinaifanya jamii iishi pamoja bila ya bughudha ili kuondoa mtu asimuonee mwingine, lakini hata kutukana ni kosa la jinai ukisoma sheria za Tanzania.
“Ukitukana mtu hapo mjini Peramiho akikupeleka polisi ukaulizwa nini kimetokea ukasema kanitukana polisi hawezi kuacha atasema eleza ilikuaje, alisemaje, mlianzaje, ndio sheria,” ameeleza Wasira.
Kwa mujibu wa Wasira, siku hizi dunia imeanza kutupa tafsiri nyingine ya uhuru, kwamba mkitukanana sana kwenye mitandao ya kijamii ndio uhuru.
“Hebu niulize wazee watuambie hivi huku katika mila na utamaduni watoto walikuwa wanatukana baba zao, walizuiwa na nani, walizuiwa na utamaduni sindio, walikuwa wanamtukana mama yao…walikuwa wamejiwekea utaratibu tofauti na demokrasia ya sasa…
“Mtoto hawezi kusema baba naye amezidi tupige kura kupata baba mwingine, hata akiwa mkorofi wanasema ah! baba naye hata akiwa mlevi wanasema baba naye karudi leo kayanywa lakini hawasemi uongozi wake unakoma wa ubaba, hapo ndipo tulipoanzia.
“Sasa unapopanua demokrasia, tena unapokuja kwenye kitu kipya kinachoitwa vyama vingi vizuri sana lakini na vyenyewe vinaweza kuwa tabu sana, lakini hakuna kisicholuwa na tabu jambo kubwa ni kuweka utaratibu ili vyama hivi vifanye kazi kwa kuzingatia katiba na sheria mliyojiwekea,” amesisitiza.