Na Mwamvua Mwinyi-
Pwani – Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Wilson Mahera, amefunga awamu ya kwanza ya mafunzo ya Utawala Bora wa Elimu kwa Maafisa Elimu Kata 346 kutoka mikoa ya Pwani na Morogoro, yaliyofanyika kwa siku tatu kuanzia Juni 11 hadi 13, 2025.
Mafunzo hayo yaliratibiwa na Wakala wa Maendeleo ya Uongozi wa Elimu (ADEM), yakilenga kuwawezesha Maafisa Elimu hao kusimamia vyema shughuli za maendeleo ya elimu katika ngazi ya kata, kwa kuzingatia misingi ya utawala bora, uwajibikaji na ufanisi.
Akizungumza wakati wa kufunga mafunzo hayo, Dkt. Mahera amepongeza juhudi za Serikali katika kuboresha elimu kupitia uimarishaji wa uongozi katika ngazi za msingi.
Mahera ameeleza mafunzo haya kutoka ADEM yamelenga kuhakikisha kuwa Maafisa Elimu wa mikoa, halmashauri na kata wanazingatia misingi ya uongozi bora na utoaji wa huduma bora za elimu.
Mtendaji Mkuu wa ADEM, Dkt. Maulid J. Maulid, amesema mafunzo hayo yataendelea kutolewa kwa Maafisa Elimu wa mikoa na halmashauri zote nchini na yamefadhiliwa na mradi wa BOOST kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia .
Lengo likiwa kuhakikisha Maafisa Elimu Kata ambao ndio viongozi, wasimamizi na washauri wa masuala yote ya kielimu katika ngazi ya kata wanapata ujuzi stahiki wa namna ya kusimamia vyema shughuli zote za kielimu zinazotekelezwa katika ngazi ya Kata kwa kuzingatia vigezo vya Utawala Bora katika elimu.
