Na Mwaandishi Wetu Mtwara
VIJANA waliojiriwa kupitia programu ya kilimo ya Jenga Kesho Iliyobora (BBT) kama maafisa ugani Mkoani Mtwara wameeleza mkakati wao wa kufanikisha lengo la serikali kuzalisha korosho tani 700,000 mwaka 2025/2026.
Maafisa hao waliajiri na Bodi ya Korosho Nchini (CBT) kupitia programu ya BBT ili kutoa huduma za kilimo, elimu na mbinu za kisasa kwa wakulima wa korosho ili kuongeza tija kwenye zao la korosho nchini.
“Kutokana na mafunzo ambayo tunapewa ninaweza kumhudumia mkulima ,kumpa elimu na mbinu za kuhudumia mikorosho, ajue namna na wakati sahihi wa kuhudumia mfano kupulizia dawa ili kuondoa visumbufu kama magonjwa kwenye mikorosho,” amesema Neema Christopher.
Naye Methew Kisum afisa ugani Wilaya ya Masasi chini ya BBT amesema “Tunapenda kuihakikishia serikali kuwa tutafanikisha lengo la kuzalisha korosho kama yalivyo matarajio Yao, tumefundishwa mbinu ,elimu na namna bora kabisa kuhudumia mkulima ili azalisha kwa tija.”
Maafisa hao walikuwa wakizungumza wakati wakipatiwa mafunzo na CBT, na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Nchini (TARI) kituo Cha Naliendele Mkoani Mtwara.
Afisa Kilimo Mwandamizi kutoka CBT Geoffrey Mwalembe maafisa hao wanapewa mafunzo ya matumizi sahihi na salama ya kutumia viautilifu vya zao la korosho ili kuwajengea uwezo wa kutoa huduma za kilimo kwa wakulima.
“Mafunzo haya ni moja kati ya malengo ya serikali kupitia Bodi ya Korosho ya kuongeza uzalishaji na tija kwenye zao la korosho kufikia tani 700,000, 2025/2026 na tani 1,000,000 mwaka 20230,” amesema.
Serikali kupitia CBT imetoa shilling bilioni 8 kutekeleza Programu ya BBT kwenye kupitia zao la korosho.