NA EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
Wahitimu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) wametakiwa kuthibitisha kwa vitendo uwezo wao walioupata chuoni kwa kutumia maarifa hayo kuleta mabadiliko chanya katika jamii na taifa kwa ujumla.
Wito huo umetolewa leo Juni 13, 2025 katika Mahafali ya 55 ya Chuo Kikuu cha Dar es Salaam yaliyofanyika kwenye ukumbi wa Mlimani City Jijini Dar es Salaam.
“Sasa ni wakati wa kuchukua hatua, kuandika, kuzungumza kwa busara na kushughulikia changamoto za jamii kwa njia bunifu na yenye maadili”. Amesema Prof. Anangisye.
Aidha amesema kuwa katika Duru ya Kwanza ya Mahafali ya 55, chuo hicho kimehudhurisha wahitimu 829 wakiwemo wa shahada ya uzamivu, shahada ya umahiri, stashahada ya uzamili, shahada ya awali, stashahada na astashahada.
Kwa upande wake, Rais na Mwenyekiti wa Bodi ya Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), Dkt. Akinwumi Ayodeji Adesina, ambaye alitunukiwa Shahada ya Heshima ya Sayansi, alieleza kuridhishwa na mwenendo wa uchumi wa Tanzania.
“Katika kipindi cha miaka 10 ya uongozi wangu kuanzia 2015 hadi 2025, AfDB imetoa msaada wa dola bilioni 4.73 kwa Tanzania, sawa na asilimia 53 ya mikopo yote ambayo benki yetu imetoa kwa nchi hiyo katika kipindi cha miaka 54,” alisema Dkt. Adesina.
“Kwa msukumo wa ukuaji katika kilimo, utalii, huduma za kifedha, uzalishaji viwandani, ujenzi wa madini sambamba na sera thabiti za mwenendo wa uchumi wa fedha, ukuaji halisi wa pato la taifa la Tanzania ukiongezeka kutoka asilimia 5.1 mwaka 2023 hadi asilimia 5.6 mwaka 2024 ” amesema.
Nae Mkuu wa UDSM, Rais Mstaafu Jakaya Kikwete amesema pamoja na hayo, Dkt. Adesina ni mdau mkubwa wa maendeleo hasa ya miundombinu.
“Huyu tuliyemtunuku benki yake ni mdau mkubwa kwa maendeleo,” amesema Kikwete.