Na Mwandishi Wetu
Akiba Commercial Plc imeonyesha dhamira yake endelevu ya kutunza mazingira kupitia zoezi la kupanda miti kwa ushirikiano na Taasisi ya Uhasibu Tanzania (TIA) katika kampasi ya Kurasini, Dar es Salaam. Miti 1,500 imepandwa kama sehemu ya mpango wa Uwajibikaji kwa Jamii (CSR) unaolenga kukuza utunzaji wa mazingira na kuimarisha ustawi wa jamii. Zoezi hilo liliongoza na Afisa Biashara Mkuu wa Benki hiyo Bi. Wezi Mwazani (Picha ya kwanza) kwa kushirikiana na wafanya kazi wengine pamoja na wanafunzi wa TIA.
Akizungumza kwa niaba ya benki katika tukio hilo, Bwana Emmanuel Mseti, Meneja Mwandamizi wa Kitengo cha Wateja Binafsi, alitoa shukrani za dhati kwa uongozi, wafanyakazi na wanafunzi wa TIA kwa mapokezi na ushirikiano mzuri uliowezesha mafanikio ya shughuli hiyo ya kimazingira. Alibainisha kuwa zoezi hili si ishara tu bali ni kitendo kinachoonyesha imani ya Benki kwamba kulinda mazingira ni jukumu la pamoja.
Benki pia ilibainisha juhudi zake nyingine za utunzaji wa mazingira ikiwemo jukumu endelevu la kutunza na kuboresha Viunga vya Independence Square jijini Dodoma. Katika tukio hilo, Bwana Mseti aliwahimiza wanafunzi wa TIA kuchukua jukumu la kulinda miti iliyopandwa na kuhakikisha inakua vizuri kwa faida ya vizazi vijavyo.
Pia aliwahakikishia kuwa Benki itaendelea kushirikiana na TIA katika kampeni za mazingira katika kampasi zake nyingine pindi itakapohitajika.
Kwa mtazamo wa Uwajibikaji kwa Jamii, Akiba Commercial inaamini kuwa kwao kurudisha kwa jamii si chaguo bali ni wajibu.
Kupitia sekta za afya, elimu, uwezeshaji wa kiuchumi, na utunzaji wa mazingira, Benki imejitolea katika maendeleo jumuishi na endelevu yanayonufaisha jamii inayoihudumia.
