Dar es Salaam, Juni 16, 2025 — Kampuni ya Multichoice
Tanzania, kupitia huduma yake ya DStv, imethibitisha dhamira yake ya kuendelea
kuwa karibu na wateja wake kwa kuzindua kampeni mpya inayojulikana kama
“Onja Utamu wa Mitanange”, ikilenga kuwawezesha wateja kushuhudia
michuano mikubwa ya FIFA kwa bei nafuu.
Akizungumza mapema leo jijini Dar es Salaam, Mkuu wa Masoko
wa Multichoice Tanzania, Ronald Shelukindo, amesema kampeni hiyo inalenga kutoa
fursa kwa kila Mtanzania, hasa wapenzi wa michezo, kupata uhondo wa michuano
hiyo mikubwa duniani LIVE, kupitia kifurushi cha bei ya chini kabisa cha POA.
“Tunatambua umuhimu wa burudani ya michezo kwa wateja wetu.
Kupitia kampeni ya ‘Onja Utamu’, sasa mteja yeyote akilipia kuanzia kifurushi
cha POA, atapata nafasi ya kujionea mechi zote za michuano ya FIFA moja kwa
moja, bila kulazimika kubadilisha kifurushi,” amesema Shelukindo.
Ameongeza kuwa lengo kuu ni kuhakikisha hakuna Mtanzania
anayekosa kushuhudia burudani hiyo ya kipekee, huku akisisitiza kuwa Multichoice
Tanzania itaendelea kuwekeza katika kuhakikisha huduma bora na zenye thamani
kwa wateja wake zinapatikana kwa kila mtu — bila kujali uwezo wa kifedha.
Kampeni ya “Onja Utamu wa Mitanange” inakuja wakati ambapo
mashabiki wa soka duniani kote wakiwa na hamasa kubwa kuelekea michuano hiyo
mikubwa ya FIFA, na hivyo kuwa fursa adhimu kwa familia, marafiki na majirani
kukusanyika pamoja na kufurahia burudani kupitia DStv.