HABARI KAMILI:
Watumishi wa umma wanaoshughulikia masuala ya sheria, malalamiko na nidhamu nchini wametakiwa kuwajibika kikamilifu kutatua changamoto za wananchi badala ya kuzipeleka kwa viongozi wa juu wa serikali, hali inayochangia mzigo usio wa lazima kwa Rais na wasaidizi wake.
Akizungumza jijini Morogoro katika mafunzo kwa baadhi ya watumishi wa taasisi za umma, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais – Ikulu, Bw. Mululi Mahendeka, alisema baadhi ya maofisa wamekuwa chanzo cha malalamiko yanayopaswa kutatuliwa kwenye ngazi za chini lakini huwasilishwa kwa viongozi wa kitaifa kutokana na uzembe au uoga wa kufanya maamuzi.
“Hatuwezi kuvumilia kuona kila tatizo la mwananchi linaishia mezani kwa Rais au Makamu wa Rais ilhali taasisi zetu zina mamlaka kamili kisheria kushughulikia hayo masuala. Mtu anayeshindwa kutekeleza majukumu yake atachukuliwa hatua kali, ikiwa ni pamoja na kuundiwa kamati ya uchunguzi,” alisema Mahendeka.
Alieleza kuwa kuanzia sasa serikali itafanya tathmini za kina kuhusu taasisi zinazozalisha malalamiko mengi na kushindwa kuyatatua kwa wakati. Taasisi hizo zitakumbwa na hatua mbalimbali, zikiwemo kuchukuliwa hatua kinidhamu kwa mujibu wa kanuni za utumishi wa umma za mwaka 2022.
“Wapo wanaoandika barua kila siku kuuliza maelekezo kwa jambo walilopewa mamlaka nalo kisheria. Huu ni uzembe. Hakikisheni mnamaliza kazi zenu kwa weledi bila kuwategemea wakubwa kuwaamulia kila kitu,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Hilda Lugembe, Mratibu kutoka Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma na Malalamiko – Ikulu, alisema mafunzo hayo ni awamu ya tatu kufanyika baada ya mikoa ya Tanga na Iringa, yakiwa na lengo la kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mashauri ya nidhamu, malalamiko, rufaa na kero za wananchi.
“Hatutaki kuona wananchi wanaandika hadi kwa Rais kwa sababu ya kitendo cha dharau au uonevu wa afisa mmoja mdogo. Hili linaipa Serikali taswira isiyo nzuri. Lengo letu ni kuhakikisha kero zinatatuliwa mapema, kwa weledi na kwa misingi ya haki,” alisema Lugembe.
Kwa upande wake, Anyangwe Lupembe, mwakilishi wa Katibu Mkuu – Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, alisisitiza umuhimu wa kila taasisi kuzingatia sheria, kanuni na miongozo katika kutoa huduma kwa wananchi. Alisema kutokufuata sheria kunasababisha hasara kwa Serikali na kupunguza imani ya wananchi.
“Ni lazima tuondokane na mazoea ya kufanya kazi kwa mazoea. Sheria ipo. Taratibu zipo. Kila mmoja asimame katika nafasi yake ili kusaidia kujenga taifa lenye uwajibikaji wa kweli,” alieleza.
Mafunzo hayo yamelenga kusaidia taasisi kuwa sehemu ya suluhisho, si chanzo cha matatizo, katika safari ya kuelekea utawala bora wenye tija kwa kila Mtanzania.
Katibu mkuu Ofisi ya Rais-Ikulu bw.Mululi Mahendeka akizungumza na baadhi ya maofisa wa taasisi za umma ambao hawapo pichani katika Mafunzo ya siku tano yalinayoendelea mkoani Morogoro.
Pichani ni Mratibu wa mafunzo hayo bi.Hilda Lugembe akizungumza wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo