Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) imesema inatekeleza mikakati mbalimbali yenye lengo la kuhakikisha upatikanaji wa gesi asilia nchini kwa matumizi mbalimbali.
Hayo yamebainishwa Juni 17, 2025 na Mkuu wa Kitengo cha Ushirikishwaji wa Wazawa na Uhusishwaji wa Wadau kutoka PURA, Bw. Charles Nyangi wakati wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea Jijini Dodoma.
“Sheria ya Petroli ya Mwaka 2015 imeipa PURA jukumu la kumshauri waziri mwenye dhamana ya masuala ya petroli katika maeneo mbalimbali ikiwemo kunadi vitalu vya utafutaji wa mafuta na gesi asilia”
“PURA imeendelea kutekeleza jukumu hili la msingi linalolenga kuvutia uwekezaji katika shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia nchini” alieleza Bw. Nyangi.
Bw. Nyangi aliongeza kuwa kupitia uwekezaji huo, shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi asilia zitaongezeka hivyo kupelekea ugunduzi wa mafuta au ugunduzi zaidi wa gesi asilia hivyo kuwezesha nchi kuwa na gesi asilia ya kutosha kwa matumizi mbalimbali.
Akizungumzia uzalishaji wa gesi asilia, Bw. Nyangi alieleza kuwa PURA imeendelea kusimamia na kudhibiti shughuli za uzalishaji wa gesi asilia kutoka katika kitalu cha Mnazi Bay kilichopo Mkoani Mtwara na Songo Songo kilichopo Mkoani Lindi.
Kupita udhibiti, PURA imewezesha kuchukuliwa kwa hatua mbalimbali zinazolenga kuhakikisha uzalishaji endelevu wa gesi asilia.
Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuwataka waendeshaji wa vitalu hivyo kufanya ukarabati wa visima kwa wakati, kuchimba visima vipya vya uzalishaji na kufanya ukaguzi wa mara kwa mara wa miundombinu ya uzalishaji wa gesi asilia.
Katika suala la uchimbaji wa visima, Bw. Nyangi alibainisha kuwa kupitia ushauri wa PURA, Kampuni ya Maurel et Prom Tanzania ambaye ni Mwendeshaji wa Kitalu cha Mnazi Bay ipo katika maandalizi ya kuchoronga visima vitatu.
Visima hivyo vitaongeza uzalishaji wa gesi asilia kwa zaidi ya futi za ujazo milioni 30 kwa siku.
PURA pia imeendelea kusimamia kuhusu maandalizi ya uchorongaji wa visima vya gesi asilia katika Eneo la Ugunduzi la Ntorya Mkoani Mtwara mbapo futi za ujazo milioni 60 hadi 140 za gesi asilia zitazalishwa kwa siku.