MUDA Africa kwa kushirikiana na Taasisi ya Nipe Fagio waliweza kuandaa tukio la Usafi wa Fukwe kwa kuadhimisha kampnei ya “Tulinde Maji Yetu”. Maonyesho ya sanaa ya dansi hayo yalifanyika katika ufukwe wa kawe na kuwaleta pamoja wananchi wa Dar es Salaam vijana, watoto, wazazi, taasisi, mashirika na watu binafsi kushiriki katika shughuli ya usafi wa fukwe na kufurahia sanaa za maonyesho zilizoandaliwa na MUDA Africa.
Tukio hili lilikuwa sehemu ya maadhimisho ya sehemu ya maadhimisho ya maonyesho ya sanaa ya dansi yanayolenga kulinda vyanzo vya maji Duniani (Global Water Dances 2025).
Hizi ni harakati ya kimataifa zinazotumia sanaa ya dansi kuongeza uelewa juu ya changamoto za maji duniani na kuhamasisha hatua za mazingira. Kaulimbiu ya mwaka huu ni “Ushirikishwaji wa Jamii kwa Ajili ya Maji Safi na Bahari Yenye Afya”, ikisisitiza umuhimu wa kushirikiana kulinda vyanzo vyetu vya maji.
Mkurugenzi wa Sanaa kutoka Muda Africa, Ian Mwaisunga alieleza, “Katika kuadhimisha siku hii, shughuli zilizopamba siku hii ni pamoja na Flash mob na kipindi cha Yoga cha pamoja,Usafi wa Ufukwe, burudani kutoka Kikundi cha Dansi cha MUDA Africa na mengine mengi.”
Tajaeli Alex Masaki kutoka Nipe Fagio aliongezea kuwa, “Sisi kama wataalamu wa mazingira tulisimamia Usafi wa Fukwe. Tulikusanya taarifa ili kupata takwimu za kutathmini ya hali ya uchafuzi wa fukwe za kawe kwa kufanya tathimini za taka na uchambuzi wa chapa za bidha kwa kitaalamu waste assessment and brand audits (WABA). Tulipata pia wasaa wa kutoa elimu ya utunzaji wa mazingira, uhifadhi na uthibiti mzuri wa taka tunazozilisha katika jamizetu.”
Sanaa, hasa dansi, zina nafasi ya kipekee katika kuchochea mabadiliko ya kijamii. Kupitia dansi, jumbe zenye mguso wa mazingira huwasilishwa kwa njia ya ubunifu, zinazoeleweka kwa urahisi na kugusa hisia.
Michael James Songoro, dancer na Mratibu wa Matukio kutoka MUDA Africa alisema:”Kushiriki usafi wa Kawe kumeleta mguso wa moja kwa moja, nimeweza kuwaelimisha jamii kupitia sanaa. Dansi ni njia ya kufikisha ujumbe kwa hisia, kwa ubunifu, na kwa lugha inayoeleweka na wote.”
Katika tukio hili, MUDA Africa wanatumia sauti na harakati kuhamasisha umma juu ya umuhimu wa kutunza bahari na vyanzo vya maji. Kwa kutumia dansi, jamii inaelimishwa, inashirikishwa, na kutekeleza hatua, hali inayooana na mkakati wetu wa kukusanya na kupatanisha data, utetezi wa sera, na kuchochea utekelezaji wa vitendo kama utumiaji wa sanaa mbalimbali kuwafikia jamii.
Tajaeli Alex Masaki mratibu wa takwimu, Nipe Fagio alisema, “Tunaposema maji ni uhai, tunamaanisha hilo kwa dhati. Tukio hili linaonyesha kwamba kupitia usafi, takwimu, na sanaa tunaweza kuwaleta watu pamoja katika harakati za kutunza mazingira yetu. Ushiriki wa jamii ndio chachu ya mabadiliko ya kweli.”
Mkurugenzi wa Sanaa kutoka Muda Africa, Ian Mwaisunga aliongeza kuwa, “Tunaamini kuwa dansi si burudani tu bali pia ni chombo cha mabadiliko. Vijana wetu wanaonesha kwa vitendo kuwa sanaa inaweza kuwa sauti ya mazingira. Ushiriki wao unatoa ujumbe wa matumaini na hatua.”
Kampeni hii imekuwa nafasi ya kipekee kwa jamii kuungana kwa ajili ya mazingira bora,afya ya bahari, na usalama wa vyanzo vyetu vya maji. Tukio hili la usafi wa Kawe na maadhimisho ya Global Water Dances 2025 limeonesha wazi kuwa jamii ikielimishwa,ikihamasishwa, na ikishirikishwa kupitia sanaa na hatua za moja kwa moja, mabadiliko chanya yanawezekana.
Faith Jacob Tarimo mwanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitoa wito kwa vijanana jamii:”Vijana tunatakiwa kuwa mstari wa mbele kulinda mazingira yetu na kushiriki katika shughuli za kijamii kama hizi. Pia, nawahimiza wanajamii kutenganisha taka zinazooza.
Zikichanganywa zinaleta madhara na changamoto ya kuzihifadhi, lakini zikitenganishwa kuanzia ngazi ya kaya, tunapata udhibiti bora wa taka tunazozalisha.”