Songea, Ruvuma
Afisa Usalama Mkuu Msaidizi kutoka Kitengo cha Uzuiaji TANESCO Makao Makuu Shami Yisuph Dunia, ametoa wito kwa wazazi na walezi kuhakikisha wanakaa na watoto wao majumbani ili kuwaonya na kuwazuia dhidi ya tabia ya kuhujumu miundombinu ya umeme, imebainika kuwa hujuma hizo hufanywa zaidi na vijana, na si wazee.
Katika ziara ya utoaji elimu iliyofanyika katika Kijiji cha Lugagala Kata ya Kilagano, Halmashauri ya Songea mkoani Ruvuma, ameeleza kuwa umeme ni hatari na kwamba ni kosa kisheria kwa mtu yeyote kufanya hujuma kwa miundombinu ya TANESCO, amesisitiza kuwa ili kujenga kizazi kinachoheshimu mali ya umma na sheria, wazazi wanao wajibu mkubwa wa kushiriki kikamilifu katika malezi na kuhakikisha watoto wao hawajihusishi na uharibifu wa miundombinu.
Vilevile, amewataka wananchi kuwa waangalifu dhidi ya watu wanaojitambulisha kama watumishi wa TANESCO ilhali si kweli, amehimiza ushirikiano baina ya jamii na shirika hilo kwa kutoa taarifa kuhusu watu wa aina hiyo, kwani kufanya hivyo husaidia TANESCO kuepuka hasara na pia kuwanusuru wananchi na changamoto ya kukosa huduma ya umeme kutokana na hujuma hizo.
Amesema TANESCO ina utaratibu wa kutoa motisha na zawadi kwa wananchi watakaotoa taarifa sahihi zinazowezesha kubainika kwa wahusika wa uharibifu wa miundombinu, zawadi hizo hutolewa kwa kuzingatia uzito wa taarifa husika, hivyo aliwasihi wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda miundombinu ya shirika.
Kwa upande wake, Alan Njiro Afisa Uhusiano na huduma kwa wateja kutoka TANESCO mkoa wa Ruvuma, ameeleza kuwa hakuna bei nyingine ya umeme vijijini zaidi ya shilingi elfu 27, amefafanua kuwa hiyo ndiyo bei rasmi kwa maeneo yote ya vijijini, hivyo wananchi hawapaswi kupotoshwa na taarifa za upotoshaji kuhusu gharama za huduma hiyo.
Akizungumza mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Halmashauri ya Wilaya ya Songea Thomas Masolwa, amelipongeza shirika hilo kwa kuendelea kutoa elimu kwa wananchi juu ya matumizi sahihi ya umeme na ulinzi wa miundombinu huku akitoa rai kwa wananchi kuendelea kuwapa ushirikiano kwa kuwafichua wahujumu ya miundombinu.