Mamlaka ya Udhibiti Mkondo wa Juu wa Petroli (PURA) ya Tanzania Bara, Mamlaka ya Udhibiti wa Utafutaji na Uchimbaji wa Mafuta na Gesi Asilia Zanzibar (ZPRA) na Mamlaka ya Petroli Uganda (PAU) zimesaini Hati ya Makubaliano inayolenga kuimarisha shughuli za utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.
Hati hiyo imesainiwa Juni 17, 2025 Jijini Entebe – Uganda katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi na wataalamu kutoka Taasisi hizo akiwemo Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PURA, Bw. Halfan Halfan na Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi ya PAU, Bi. Lynda Biribonwa.
Viongozi wengine walioshiriki hafla hiyo ni pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa PURA, Mha. Charles Sangweni, Mkurugenzi Mtendaji wa PAU, Mha. Ernest Rubondo na Mkurugenzi Mwendeshaji wa ZPRA, Mha. Muhammed Said.
Kwa mujibu wa Hati iliyosainiwa, PURA, PAU na ZPRA zimekubaliana kushirikiana katika maeneo ya usimamizi wa rasilimali za mafuta na gesi asilia, usimamizi wa data za petroli na ukaguzi wa gharama.
Maeneo mengine ni ushiriki wa wananchi katika miradi ya mafuta na gesi asilia; afya, usalama, na mazingira; na uandaaji wa sheria, kanuni na miongozo inayohusiana na utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia.
Akizungumza katika halfa ya utiaji saini, Mwenyekiti wa Bodi ya PURA, Bw. Halfani Halfani alisema suala la kubadilishana uzoefu na kujengeana uwezo baina ya Taasisi hizo ni muhimu kwa ustawi wa tasnia ya mafuta na gesi asilia nchini Tanzania na Uganda.
“kupitia makubaliano haya, ni dhahiri kuwa shughuli za ufafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi asilia katika nchi zetu zinakwenda kuimarika” alisema Halfani.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya PAU, Bi. Lynda Biribonwa alieleza umuhimu wa wadhibiti kushikiana ili kuleta maendeleo endelevu ya rasilimali za mafuta na gesi asilia katika ukanda wa Afrika Mashariki.