Na Janeth Raphael MichuziTv -Dodoma
Bilioni 1.7 zimetolewa kwa ajili ya kusaidia matibabu ya ugonjwa wa seli mundu kwa wagonjwa wanaojitokeza kupata matibabu mbalimbali katika hospitali ya Rufani ya Kanda ya Benjamini Mkapa (BMH).
Mkurugenzi wa Hospitali ya Rufani ya Kansa ya Benjamini Mkapa (BMH),Profesa Abel Makubi ameyaeleza hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya seli mundu duniani yanayoazimishwa kila mwaka Juni 19.
Aidha jamii imeiomba serikali kuangalia namna ya kupunguza gharama za matibabu ya ugonjwa huo ambapo gharama ya mgonjwa mmoja ni sh milioni 75 ambayo ni kubwa sana familia mbalimbali kuimudu.
Profesa Makubi amesema Serikali inafanya jitihada kubwa sana za kuhakikisha inakabiliana na ugonjwa huo ndio maana inatoa fedha za kununua dawa pamoja na vifaa tiba mbalimbali ili kuhakikisha wagonjwa wanaojitokeza wanapata tiba.
“Serikali inapambana kila siku kuhakikisha ugonjwa huo unapata tiba,ndio maana inafanya uwekezaji wa fedha kwa ajili ya matibabu mbalimbali kwa wagonjwa wa Selimundu,”alisema Profesa Makubi.
Prof Makubi amesema mpaka sasa tayari wamepandikizwa uloto kwa wagonjwa zaidi ya 20 na wanaendelea vizuri kutokana na matibabu hayo.
“Tunamshukuru Rais Samia na Serikali kwa ujumla kwa uwekezaji huo mkubwa kwa ajili ya matibabu ya watoto wenye ugonjwa huo na tukiwa tunaadhimisha siku hii ya seli mundu duniani tunafuraha kusema kuwa mpaka sasa tumetibu watoto 21 na wamepona kabisa na bado tunaendelea kutoa matibabu kwa watoto wengine lengo ni kutokomeza kabisa ugonjwa huu,” amesema Prof. Makubi.
“Sisi kama BMH tunahakikisha katika kutoa elimu ya uelewa kwa wananchi na kuondoa dhana potofu ambazo zipo katika jamii katika vijiji na miji mbalimbali kwa kufanya huduma mkoba,” ameongeza Prof. Makubi.
Kwa upande wake Dkt. Shakiru Jumanne ambae ni Amidi shule kuu ya Tiba katika chuo kikuu cha Dodoma (UDOM) na pia daktari bingwa wa magonjwa ya damu amesema kuwa UDOM itaendelea kuzalisha wataalamu na kufanya tafiti mbalimbali kwa ajili ya kupata matibabu ya ugonjwa huu.
“Chuo kikuu cha UDOM kinaendelea kuzalisha wataalamu ambao watasaidia katika kutoa huduma kwa wagonjwa wa selimundu lakini pia kufanya tafiti ili kugundua matibabu zaidi na namna ya kudhibiti ugonjwa huu,” amesema dkt. Shakiru.
Mmoja wa wazazi ambao mtoto amepandikizwa uloto kutibu selimundu ambaye ni Mkazi wa Iyumbu Mary Consolata Mkungano aliyefuatana na Prof.Mkubi katika mkutano wa waandishi wa habari alisema;
“Gharama za kutibu mgonjwa mmoja ni kubwa sana sh milioni 75 mtu pekeyake hawezi kulipa,hivyo serikali iangalie namna ya kuisaidia jamii kuhusiana na matibabu hayo kwa sababu yanazitesa familia,”alisema Mkungano