Songea_Ruvuma.
Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kupitia ofisi yake ya Mkoa wa Ruvuma, limewasihi wateja wake wenye madeni kuhakikisha wanalipa madeni yao hususan katika kipindi hiki cha mavuno, ili kuwezesha shirika hilo kuendelea kusambaza huduma ya umeme kwa maeneo ambayo bado hayajafikiwa.
Wito huo umetolewa na Afisa Uhusiano na Huduma kwa Wateja wa TANESCO Mkoa wa Ruvuma Alan Njiro, akiwa katika kata za Liganga, Litisha na Maposeni, zilizopo katika Halmashauri ya Wilaya ya Songea.
Njiro amesema kuwa kipindi cha mavuno ni muda muafaka kwa wateja kulipa madeni yao kutokana na mapato yanayotokana na mauzo ya mazao. Amefafanua kuwa mapato hayo yakitumika kulipia madeni, yatasaidia shirika kuimarisha utoaji wa huduma kwa maeneo mengine yanayohitaji umeme.
“Tunashauri kila mteja kuhakikisha ananunua umeme kila mwezi, hata kwa kiwango kidogo. Hii itasaidia kulipa madeni na kuiwezesha TANESCO kutekeleza miradi ya upanuzi wa huduma kwa wananchi wengi zaidi,” alisema Njiro.
Aidha, amewaasa wananchi kuwa wazalendo kwa kutoa taarifa pale wanapobaini uwepo wa watu wanaotumia umeme bila kulipia kupitia mita halali. Alisisitiza kuwa wizi wa umeme ni kosa kisheria, na TANESCO kwa kushirikiana na vyombo vya usalama, itachukua hatua kali za kisheria dhidi ya wahusika.
Njiro pia aligusia changamoto ya wateja waliokuwa wakitumia mita za zamani, ambao madeni yao yamehamishiwa kwenye mita za LUKU. Baadhi ya wateja hawa wameacha kununua umeme, jambo linalosababisha madeni yao kutolipika, amesisitiza kuwa ni muhimu waendelee kununua umeme ili madeni hayo yalipwe kidogo kidogo kupitia mfumo wa LUKU.
Kwa ujumla, TANESCO imeendelea kuhimiza wateja wake kutimiza wajibu wao wa kulipa madeni, si tu ili kuepuka usumbufu wa kukatiwa huduma, bali pia kuchangia jitihada za kitaifa za kuhakikisha huduma ya umeme inawafikia Watanzania wote kwa usawa na kwa wakati.