![]() |
Takribani wakulima 30 kutoka vijiji mbalimbali vya Wilaya ya Chemba na Kondoa wamejengewa uwezo kupitia mafunzo ya vitendo ya kilimo rafiki kwa mazingira, ikiwa ni sehemu ya ziara ya mafunzo ya siku tatu iliyofanyika katika Chuo cha Ufundishaji na Utafiti cha Sustainable Agriculture Tanzania (SAT), kilichopo mkoani Morogoro.
Mafunzo hayo yamewezeshwa na mradi wa Bread for the World unaotekelezwa na shirika la INADES-Formation Tanzania, kwa lengo la kuwaimarisha wakulima katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi kupitia mbinu bora za kilimo na ufugaji endelevu.
Wakiwa chuoni hapo, wakulima walijifunza mbinu mbalimbali ikiwemo kilimo hai, kilimo janja, kilimo ikolojia na kilimo msitu, huku wakishiriki kwa vitendo katika uandaaji wa bustani jiko, ujenzi wa mifereji ya kuvuna maji ya mvua, na utengenezaji wa mboji.
Mtaalamu wa kilimo kutoka SAT, Bw. Jackson Mkonji, aliwaongoza wakulima hao kwa kuwafundisha hatua kwa hatua kuhusu uandaaji wa vitalu vya miti, utengenezaji wa dawa za asili kwa ajili ya kudhibiti wadudu waharibifu kwa kutumia mimea kama mwarubaini, pilipili, utupa, na majani ya nyanya. Pia walifundishwa namna ya kutengeneza mboji bora inayochochea uzalishaji wa mazao bila kutegemea mbolea na viuatilifu vya viwandani.
Meneja wa chuo hicho, Bi. Angelina Mbele, aliwahimiza wakulima kuzingatia matumizi ya mbegu za asili kama vile mahindi ya Situka, ili kupunguza utegemezi wa mbegu za viwandani na kuongeza uhuru wa uzalishaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa INADES-Formation Tanzania alisema kuwa lengo la mafunzo hayo ni kuwawezesha wakulima kuendesha kilimo na ufugaji kama biashara, kwa kuongeza tija, kuimarisha masoko ya mazao yao na kutambua fursa zilizopo katika sekta ya kilimo.
“Tunatambua kuwa kilimo ni injini ya maendeleo kwa jamii ya vijijini, na kupitia mafunzo haya, wakulima wataweza kulima kwa tija, kupata kipato bora na kwa wakati huo huo kulinda mazingira na afya ya mlaji,” alisema.
Wakulima walioshiriki walieleza shukrani kwa INADES-Formation Tanzania kwa kuwawezesha kupata maarifa mapya yatakayobadilisha maisha yao na kukuza uchumi wa familia zao.
Katika ziara hiyo, wakulima waliambatana na maafisa wa kilimo na ufugaji pamoja na afisa ustawi wa jamii kutoka wilaya za Chemba na Kondoa.