Halmashauri ya Wilaya ya Madaba imepongezwa kwa kuwa miongoni mwa Halmashauri 10 bora kati ya 185 nchini Tanzania zinazotekeleza kwa ufanisi mkubwa usimamizi wa masuala ya lishe.
Pongezi hizo zimetolewa na Mkuu wa Wilaya ya Songea, Mhe. Kapenjama Ndile, wakati wa kikao cha tathmini ya mkataba wa lishe kwa robo ya pili ya mwaka wa fedha 2024/2025, kilichofanyika katika Ukumbi wa Halmashauri hiyo.
Akizungumza katika kikao hicho, Mhe. Ndile aliwapongeza watumishi wote wa Halmashauri kuanzia ngazi ya vitongoji, vijiji, kata hadi ngazi ya Halmashauri kwa kazi kubwa wanayoifanya katika kuhakikisha wanafunzi wanapata chakula bora chenye virutubisho muhimu vya lishe, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kupambana na changamoto ya lishe duni miongoni mwa watoto.
Kwa upande wake, Afisa Lishe wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, Ndg. John Mapunda, alieleza baadhi ya mafanikio yaliyofikiwa, ikiwemo kufunguliwa kwa mashine tatu za kuongeza virutubisho kwenye unga wa mahindi ili kuhakikisha jamii inapata lishe bora kupitia vyakula vya kila siku.
Aidha, kupitia Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Halmashauri imeanzisha mashamba ya mfano ya mahindi ya njano katika shule sita za msingi na shule nne za sekondari kama sehemu ya utekelezaji wa programu ya chakula shuleni. Vilevile, idara ya Elimu ya Msingi na Sekondari imeendelea kuhamasisha wazazi kuchangia vyakula kwa ajili ya wanafunzi shuleni.
Katika kuhakikisha masuala ya lishe yanapewa kipaumbele, Halmashauri ya Madaba imeweka mikakati ya kuendelea kutoa elimu kwa jamii kuhusu matumizi ya vyakula vilivyoongezewa virutubisho na kufanya tathmini ya mara kwa mara ili kubaini watoto wenye changamoto za lishe na kuwapatia huduma stahiki.
Kwa mwaka wa fedha 2025/2026, Halmashauri imetenga fedha katika bajeti ya idara ya kilimo na elimu kwa ajili ya ununuzi wa mbegu za mahindi ya njano pamoja na mbegu za mazao ya bustani ili kuendeleza jitihada za kuboresha lishe kwa wanafunzi na jamii kwa ujumla.