Madaba_Ruvuma.
Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Mkoani Ruvuma, imekanusha taarifa inayosambaa katika mitandao ya kijamii na baadhi ya majukwaa ya habari kupitia kipande cha video (video clip), zikionyesha na kudai uwepo wa shule ya Msingi inayoitwa Litepatile yenye changamoto ya miundombinu ya madarasa na uhaba wa waalimu kuwa sio za kweli na zipuuzwe kwani Halimashauri hiyo haina shule iliyosajiliwa kwa jina hilo.
Kupitia taarifa yake kwa umma Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Madaba Wilayani Songea Mkoani Ruvuma Sajidu Idrisa Mohamed, inawataka wananchi na Watanzania wote kupuuza taarifa hizo zinazoashiria lengo la upotoshaji na kuchafua taswira ya serikali na kudhoofisha juhudi za maendeleo zinazotekelezwa kikamilifu Wilayani humo.
Taarifa inaeleza mnamo Aprili 24 mwaka 2022, aliyekuwa Mkuu wa Mkoa wakati ule Brigedia Jenerali Balozi Wilbert Augustine Ibuge, alitoa kauli rasmi kupitia JEMEDARI TV, akikaunusha taarifa hiyo hiyo ya video inayosambazwa hivi sasa na kueleza kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote na akatangaza msako mkali dhidi ya wote waliohusika kusambaza upotoshaji huo.
Ibuge alitangaza msako mkali dhidi ya wote waliohusika kusambaza upotoshaji huo wa kipande cha video na ili kujiridhisha na mahojiano ya kipindi hicho wananchi wanatakiwa kutembelea YouTube kupitia kiunganishi cha JEMEDARI TV kujionea taarifa iliyochapishwa tarehe 24 Aprili mwaka 2022 ikionyesha wazi msimamo wa serikali juu ya suala hili.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo Mkurugenzi Mtendaji Mtendaji wa Halmashauri ya Madaba, anawakumbusha wanahabari, watumiaji wa mitandao ya kijamii na wananchi wote kwamba, ni wajibu wa msingi kuthibitisha taarifa kutoka pende zote kabla ya kusambaza kwa umma.
Kusambaza uzushi ni kosa la jinai chini ya sheria ya Makosa ya mtandao Na. 14 ya mwaka 2015, na hatua kali zitachukuliwa kwa wote watakaobainika chini ya kifungu cha 16 ambacho kinakataza kusambaza taarifa za uongo kwa nia ya kupotosha umma, kifungu cha 20 kinaharamisha matumizi ya mitandao kusambaza taarifa zisizothibitisha na zenye madhara kwa jamii, Mkurugenzi ameeleza kuwa mtu yoyote atakaebainika kusambaza taarifa na video hiyo, hatua kali za kisheria zitachukuliwa dhidi yake kwa kukiuka masharti yaliyoainishwa.
Halmashauri ya Wilaya ya Madaba imesema serikali ya Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania imetekeleza miradi ya maendeleo kupitia ilani ya uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi CCM ya mwaka 2020-2025, fedha nyingi kutoka serikali kuu zimesaidia kukamilisha miradi ya kimkakati inayogusa maisha ya Watanzinia, na kuahidi kuendelea kushirikiana na kusimamia kwa makini utekelezaji wake wa majukumu kwa masilahi mapana ya wananchi.