Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) umetakiwa kuyatumia vyema maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma kwa kuelimisha watumishi wa umma juu ya huduma na miradi mbalimbali inayotekelezwa na taasisi hiyo, hususan katika sekta ya makazi na ujenzi wa ofisi.
Wito huo umetolewa na Katibu Mkuu wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Bw. Juma Selemani Mkomi, alipotembelea banda la TBA katika viwanja vya Chinangali, jijini Dodoma, ambako maonesho hayo yanaendelea.
“Kwenye maonesho haya mmekuja kuonesha huduma mnazotoa, ambazo zinawahusu sana watumishi wa umma. Hao ndio wahitaji wakuu wa makazi, ofisi na maeneo mengine ya matumizi. Ni vyema mkatoa maelezo ya kutosha kuhusu huduma zenu ili ziweze kufahamika kwa urahisi,” amesema Bw. Mkomi.
Ameongeza kuwa bado kuna changamoto ya uelewa kwa baadhi ya watumishi wa umma kuhusu mahali wanapoweza kupata nyumba za makazi, hivyo amesisitiza TBA kuongeza jitihada za kuhamasisha na kutoa elimu kwa watumishi kuhusu upatikanaji wa huduma hizo.
Kwa upande wake, mmoja wa watumishi wa umma waliotembelea banda hilo, Bw. Hussein Mzee Mussa, amesema ameridhishwa na miradi mbalimbali ya nyumba inayotekelezwa na TBA, ikiwemo mradi mkubwa wa ujenzi wa nyumba 3,500 za makazi unaoendelea katika eneo la Nzuguni jijini Dodoma.
“Mradi huu ukikamilika utasaidia kwa kiwango kikubwa kupunguza changamoto ya makazi kwa watumishi wa umma hapa mkoani Dodoma,” amesema Bw. Mussa.
TBA inaendelea kutumia maonesho ya wiki ya utumishi wa umma kama jukwaa la kuelezea miradi ya ujenzi na ushauri inayoitekeleza, ikiwemo ya nyumba za makazi kwa watumishi wa umma, ujenzi wa ofisi za serikali, pamoja na ujenzi wa mji wa serikali unaoendelea jijini Dodoma.