Na Mwandishi Wetu
KAMPUNI ya Tanzania Breweries Plc (TBL) kwa kushirikiana na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI), wameandaa tukio la kuwakutanisha wadau wa zao la mtama wakiwemo wakulima,viongozi wa serikali za mitaa, watafiti.
Katika tukio hilo wadau hao kwa pamoja wamepata nafasi ya kuonesha ubunifu, ushirikiano na mafanikio ya kilimo bora huku kauli mbiu ikiwa inasem “Shangwe kwa wakulima!” ambayo imelenga kuonesha uhusiano wa muda mrefu kati ya TBL na wakulima zaidi ya 2,400 walioko katika mpango wa ununuzi wa mtama kwa msimu wa kilimo wa mwaka 2025.
Mpango huo ndio dira kwa manunuzi ya malighafi za ndani ya kampuni . Kwa ujumla, ABINBEV kampuni mama ya TBL inashirikiana na zaidi ya wakulima 20,000 katika mnyororo mzima wa thamani, ambapo zaidi ya asilimia 68 ni wakulima wadogo.
Mpango huo umejikita katika kuwajengea uwezo wakulima kupitia mafunzo, upatikanaji wa takwimu, zana na teknolojia ili kuwasaidia kufanya maamuzi bora. Tunafanya kazi kwa karibu na wakulima kutatua changamoto shambani na kutoa suluhisho kulingana na mazingira yao.
Akizungumza wakati tukio hilo la TBL na TARI ambao pia wameshirikiana kuadhamisha Siku ya Wakulima wa Mtama Hombolo mkoani Dodoma Katibu Mkuu wa Wizara ya Kilimo, Gerald Mweli aliyekuwa mgeni rasmi amesema alisema ushirikiano kati ya sekta ya umma na binafsi kama huo ni muhimu kwa mageuzi ya sekta ya kilimo.
“Ushirikiano kati ya TBL, TARI na wakulima wa Hombolo unaonesha jinsi maarifa, teknolojia na uwekezaji vinavyoweza kuleta usalama wa chakula, mafanikio ya kiuchumi, na maendeleo ya taifa.”
Wakati wa hafla hiyo, wakulima walipewa taarifa kuhusu utafiti wa hivi karibuni, teknolojia za kisasa za kilimo na ubunifu unaoungwa mkono na AB InBev, ikiwa ni pamoja na maonesho ya moja kwa moja ya mashine mpya ya kupanda mtama na mbinu bora za upandaji zilizowasilishwa na TARI.
Kwa huo huo Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin, amesema tukio hilo linaonesha dhamira yao ya dhati kwa wakulima wa ndani na kilimo endelevu na kusisitiza wanajivunia kuunga mkono ubunifu unaosaidia kuongeza uzalishaji na kubadilisha maisha.
“Ushirikiano wetu na TARI na msaada endelevu kutoka kampuni mama yetu, AB InBev, unatuwezesha kuendelea kuwekeza kwenye yale yanayowagusa zaidi watu wa jamii zetu.”
Pia amesema TBL imetoa mashine za kupandia na kupigia mtama kwa vikundi mbalimbali vya wakulima wa Mtama . Lengo likiwa ni kuzuia upotevu wa mtama wakati wa kuvuna pia kurahisisha shughuli za upandaji wa mtama na kuongeza tija katika uzalishaji.
“Siku ya Wakulima wa Mtama pia imeonesha jinsi TBL inavyojipanga kufanikisha Malengo ya Maendeleo Endelevu (SDGs), hususan katika kutokomeza njaa kwa kuimarisha usalama wa chakula kupitia tija ya kilimo.”
Pia matumizi ya uzalishaji endelevu kupitia ununuzi wa mazao endelevu na mbinu bora za kilimo, hatua dhidi ya mabadiliko ya Tabianchi kwa kutambulisha teknolojia rafiki kwa mazingira na ushirikiano wa maendeleo kwa kupitia ushirikiano wa maana na taasisi kama TARI.
Kwa upande wa TARI, Dkt. Deusdedith Mbazibwa akimuwakilisha Mkurugenzi wa TARI alisema: “Ushirikiano wetu na TBL umejikita katika ubunifu unaotokana na uzoefu wa moja kwa moja mashambani.
” Kuanzia majaribio ya mbegu hadi kwenye matumizi ya mashine, lengo letu ni kuwawezesha wakulima kwa teknolojia inayotegemea sayansi na inayolenga matokeo. Tukio hili linaonesha jinsi teknolojia na mbinu bora za kilimo zinavyoweza kuinua maisha ya vijijini.”
Maadhimisho ya Siku ya Wakulima wa Mtama yamehitimishwa kwa ahadi ya pamoja kutoka kwa wadau wote wa kuendelea kupanua wigo wa elimu ya kilimo na teknolojia ili kuongeza tija, kipato na ustawi wa jamii za wakulima kote nchini.