Halmashauri ya Wilaya ya Geita, inajivunia kukusanya mapato yanayofikia zaidi ya shilingi bilioni 10 mpaka hadi kufikia juni 20 2025 ambapo inatafsiriwa sawa na kuvuka lengo katika ukusanyaji wa mapato katika halmashauri hiyo.
Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hiyo Karia Rajabu Magaro ameyasema hayo wakati wa kikao cha kuvunja baraza la madiwani ambapo amesema kuwa mapato hayo ni sawa na asilimia 120.62 na kwamba suala hilo ni la kujivunia.
Magaro ameongeza kuwa mapato hayo yanatokana na na ushirikiano alioupata kutoka kwa madiwani na watendaji wengine katika halmashauri hiyo.
Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Geita Charles Kazungu amesema kuwa baraza kuvunjwa isiwe mwisho wa watendaji wa halmashauri kujituma na kuendeleza juhudi zilizoachwa na madiwani waliokamilisha kazi yao mnamo juni 20 mwaka huu.
Meneja wa RUWASA Wilaya ya Geita Mhandisi Sande Batakanwa, amesema kwa kipindi Cha Miaka mitano, katika Wilaya ya Geita kulikuwa na miradi minne ambayo ni Mharamba, Chankorongo, ruhuha na Nyakagomba.
Lakini kipindi hiki kifupi, wamejenga miradi zaidi ya 22, na kwamba bado kuna programu ambazo zinaendelea.
Naye Meneja wa TARURA Wilaya ya Geita Mhandisi Bahati Subeya, amewashukuru Madiwani kwa ushirikiano wao katika kipindi Cha Miaka mitano ambapo amedai kuwa kwa kipindi chote walikuwa na mikataba 35, na Halmashauri ya Wilaya Geita pekee ilikuwa 20 na 17 imekamilika ikiashiria kwamba kazi kubwa imefanyika.
Ameongeza kuwa 2024/2025 kulikuwa na mikataba 25, huku 14 ikiwa ya Halmashauri ya Wilaya ya Geita na mikataba Saba imekamilika.