Na Mwandishi Wetu, Accra
Juni 24, 2025
Kamishna wa Uhifadhi wa Wakala wa Huduma za Misitu Tanzania (TFS), Profesa Dos Santos Silayo, ameongoza kikao cha Baraza la Uongozi la Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Barani Afrika (African Forestry and Wildlife Commission – AFWC) kinachofanyika kwa siku tatu jijini Accra, Ghana.
Kikao hicho kimewakutanisha viongozi waandamizi kutoka nchi wanachama wa Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO) kwa lengo la kujadili maendeleo, changamoto na mikakati ya pamoja ya kuimarisha usimamizi endelevu wa misitu na wanyamapori barani Afrika.
Pia kinatumika kuandaa mkutano wa 25 wa Kamisheni hiyo, unaotarajiwa kufanyika baadaye mwaka huu sambamba na maadhimisho ya Wiki ya Misitu na Wanyamapori Afrika.
Akizungumza wakati wa ufunguzi, Profesa Silayo ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamisheni hiyo na Makamu Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Misitu (Committee on Forestry – COFO) alisema Kamisheni hiyo ni jukwaa muhimu kwa nchi za Afrika kujadili sera, mafanikio na changamoto zinazokabili sekta ya misitu na wanyamapori.
Alisisitiza kuwa AFWC pia ina jukumu la kushauri FAO na nchi wanachama kuhusu sera, mipango na mbinu bora za usimamizi wa rasilimali hizo kwa kuzingatia mahitaji ya kikanda.
Aliongeza kuwa Kamisheni hiyo huchochea ushirikiano wa kikanda baina ya nchi za Afrika katika nyanja za uhifadhi na matumizi endelevu ya misitu na wanyamapori, na hufuatilia utekelezaji wa mikataba ya kimataifa kama vile Mkataba wa Umoja wa Mataifa kuhusu Mabadiliko ya Tabianchi (UNFCCC), Mkataba wa Bioanuwai (CBD), na Mpango wa Kupunguza Uzalishaji wa Hewa Ukaa (REDD+).
Aidha, Kamisheni huwasilisha msimamo wa pamoja wa Afrika katika maamuzi ya Kamati ya Kimataifa ya Misitu (COFO).
Profesa Silayo alibainisha kuwa kikao hicho ni fursa adhimu kwa bara la Afrika kufanya tathmini ya utekelezaji wa sera mbalimbali na kuweka mikakati ya kuimarisha ushirikiano wa kikanda kwa manufaa ya sasa na ya vizazi vijavyo.
Alisisitiza kuwa katika kipindi hiki cha changamoto za kimazingira, ongezeko la watu na shinikizo kwa rasilimali asilia, bara la Afrika linahitaji kuwa na msimamo mmoja na hatua madhubuti za pamoja.
Miongoni mwa viongozi walioungana na Profesa Silayo katika kikao hicho ni Abbey Haile Gabriel, Mkurugenzi Msaidizi wa FAO Kanda ya Afrika; Pierre Taty, Mwenyekiti wa Kamati ya Kimataifa ya Misitu (COFO); Profesa Labode Popoola, Katibu Mtendaji wa Jukwaa la Misitu Afrika (AFF); na Edward Kilawe, Katibu wa Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Afrika.
Kamisheni ya Misitu na Wanyamapori Afrika (AFWC) ni chombo cha kikanda kilichoanzishwa chini ya FAO kwa madhumuni ya kuratibu, kushauri na kuendeleza usimamizi endelevu wa misitu na wanyamapori katika bara la Afrika. Makao yake makuu yapo katika Ofisi za FAO Kanda ya Afrika jijini Accra, Ghana. Kwa sasa, Kamisheni hiyo inaongozwa na Tanzania kupitia Profesa Silayo, hatua inayoakisi mchango mkubwa wa nchi katika majukwaa ya kimataifa ya uhifadhi wa mazingira na matumizi endelevu ya rasilimali za misitu