Na. Mwandishi Wetu
Watendaji wa uboreshaji wa Daftari la Kudumu
la Wapiga Kura kwenye Magereza kwa Tanzania Bara na Vyuo vya Mafunzo kwa
Tanzania Zanzibar wametakiwa kuzingatia mafunzo waliyopatiwa na Tume Huru ya
Taifa ya Uchaguzi (INEC) ili waweze kutekeleza zoezi hilo kwa ufanisi.
Wito huo umetolewa na Mjumbe wa INEC, Mhe.
Balozi Omar Ramadhan Mapuri mkoani Dodoma leo tarehe 24 Juni, 2025 wakati
akifunga mafunzo kwa Waratibu, Waandishi Wasaidizi na Waendesha Vifaa vya
Bayometriki wa magereza ya Tanzania Bara.
Mafunzo hayo ya siku tatu yamefanyika
sambamba na mafunzo ya watendaji wa vyuo vya mafunzo kwa upande wa Tanzania
Zanzibar ikiwa ni maandalizi ya kuandikisha na kuboresha taarifa za mahabusu,
wafungwa na wanafunzi waliohukumiwa kifungo chini ya miezi sita.
“Ikumbukwe kwamba, mafunzo na maelekezo
mliyopewa ni zana muhimu za kuwawezesha kutekeleza kwa ufanisi majukumu yenu.
Hivyo, mnatakiwa kuyafahamu vizuri na kuyafuata ili kutekeleza zoezi hili kwa
ufanisi. Someni kwa makini vitabu vya maelekezo mlivyopatiwa ili kazi yenu
ifanyike kwa usahihi,” amesema Mhe. Mapuri.
Amewasisitiza watendaji hao juu ya umuhimu wa
kuwasiliana na waratibu kwa ajili ya ufafanuzi wa masuala yote yanayohusiana na
utekelezaji wa majukumu yao.
Akifunga mafunzo kama hayo kwa watendaji wa
vyuo vya mafunzo yaliyofanyika Kisiwani Unguja, Zanzibar, Mjumbe wa Tume Huru
ya Taifa ya Uchaguzi, Mhe. Jaji wa Mahakama Kuu, Asina Omari amewaasa watendaji
hao kuhakikisha kuwa wanavitunza vizuri vifaa vya uboreshaji wa Daftari.
“Mnasisitizwa kuzingatia kwa umakini utunzaji
wa vifaa vya uandikishaji kwa kuwa vifaa hivi vimenunuliwa kwa gharama kubwa
sana. Kutokuwa makini katika utunzaji wa vifaa hivi kutapelekea athari kubwa ya
vifaa hivyo muhimu kwa Taifa,” amesema Jaji Asina.
Amewakumbusha watendaji hao juu umuhimu wa
kuzingatia muda sahihi wa kufungua na kufunga vituo vya kuandikisha wapiga kura
na kuongeza kuwa watendaji hao wanapaswa kuwa na matumizi ya lugha nzuri kwa
wale watakaowahudumia vituoni.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Tume, zoezi
hilo la uboreshaji wa Daftari kwenye Magereza na Vyuo vya Mafunzo linafanyika
kwa siku saba kuanzia tarehe 28 Juni hadi tarehe 04 Julai, 2025 ambapo
watakaohusika ni mahabusu na wafungwa walihukumiwa kifungo chini ya miezi sita.
Wajumbe wa Menejiment ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi wakiwa jkatika Mafunzo hayo mjini Dodoma.